Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma atoa pongezi kwa Madiwani
Na. Nancy Kivuyo, DODOMA
Mstahiki
Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe, amelipongeza Baraza
la Madiwani kwa kazi nzuri ya usimamizi wa miradi ya maendeleo katika kata zao iliyopelekea
uboreshaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.
Aliyazungumza hayo katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri wakati wa mkutano wa Baraza la Madiwani wa kupitia taarifa za utekelezaji kutoka kwenye kata 41 za Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Alisema
kuwa madiwani wamesimamia vizuri miradi ya maendeleo iliyotekelezwa katika kata
zote 41. “Sisi Halmashauri ya Jiji la Dodoma tulipanga kukusanya na kutumia
shilingi bilioni 143, kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 62.3 ni za mapato ya
ndani. Kupitia mapato ya ndani tumetenga vilevile, kwa kuzingatia taratibu zetu
asilimia 70 itumike kwenda kutekeleza miradi ya maendeleo. Kwa muktadha huo, ni
busara sana tuwe na taarifa miradi hiyo imetekelezwaje” alisema Prof. Mwamfupe.
Aliongeza
kuwa katika mkutano huo wa robo ya tatu walijikita katika kupitia miradi iliyotekelezwa
katika kata zote na akawapongeza madiwani kwa kusimamia vizuri miradi hiyo.
“Tumeangazia miradi ya aina mbili, moja ni ile miradi ilianzishwa kwa nguvu za
wananchi na pili ni miradi viporo ambayo kwa kuikamilisha inatakiwa kutumika
mara moja. Miradi imetekelezwa vizuri. Kwa mfano, ujenzi wa Shule ya Sekondari
Matumbulu pamoja na changamoto zilizopo lakini wamefanya vizuri na miradi
mingine nawapongeza sana” aliongeza Prof. Mwamfupe.
Alimalizia kwa kusema kuwa ana furaha kuona madiwani wanasimamia vilivyo utekelezwaji wa miradi ya maendeleo na kuwa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi ni wakati muafaka wa kueleza kuwa serikali imefanya yapi kwa wananchi. Bila kusahau akatoa pongezi kwa wananchi na juhudi za michango yao katika kuihimiza serikali kusogeza huduma katika maeneo yao.
Naye
Diwani wa Kata ya Kiwanja cha Ndege, Amos Mbalanga alisema kuwa mkutano huo umekuwa
na matokeo chanja kwao kwasababu wameweza kufahamu namna miradi mbalimbali ilivyotekelezwa.
“Kipekee nilipongeze baraza kwasababu katika robo ya tatu hii tumepata taarifa
za namna miradi ilivyotekelezwa kwa wingi, tutaendelea kuisimamia miradi kikamilifu
ili kusogeza karibu huduma kwa jamii na hilo ndio lengo letu” alisema Diwani
Mbalanga.
Katika
hatua nyingine, Diwani wa Viti Maalum, Flora Liacho alieleza kuwa mapitio ya
miradi ya maendeleo ni jambo zuri kwasababu linawafanya madiwani kuwajibika.
“Nalipongeza Baraza la Madiwani kwakuwa na desturi ya kukutana kila baada ya
robo ya tatu kwasababu kama leo hii tumejadili namna miradi ya maendeleo
inatekelezwa katika kata na tumeiona ile miradi kinara iliyokamilika na ipo
ambayo bado ni viporo. Naamini wanaosimamia hiyo miradi viporo wataongeza kasi
ikamilike kwa wakati ili wananchi wapate huduma” alipongeza Diwani Liacho.
MWISHO
Comments
Post a Comment