Wanufaika wa mkopo wasisitizwa kufanya marejesho kwa wakati
Na. Aisha Ibrahim, UHURU
Afisa Maendeleo ya Jamii, Kata ya Uhuru, Saada Zahaze,
amewasisitiza wanufaika wa mkopo wa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye
ulemavu kuzingatia miongozo na sheria za utoaji mkopo ikiwa ni kutumia fedha
hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na kufanya marejesho kwa wakati uliopangiwa
kupitia mfumo jumuishi.
Mfumo huo jumuishi unatekelezwa kwa mujibu wa sheria kwa kutoa mikopo ya asilimia 10 katika Jiji la Dodoma kwa uwiano wa 4-4-2 yaani wanawake asilimia nne, vijana asilimia nne na watu wenye ulemavu asilimia mbili.
Akitoa ufafanuzi kuhusu mgawanyo wa mikopo hiyo alisema kuwa
Kata ya Uhuru wamesajili vikundi 52, kati ya hivyo 18 ni vya wanawake, 17 ni
vijana na 17 ni vya watu mchanganyiko ambapo katika vikundi hivyo, 18 tayari
vimeshapata mkopo huo.
Aliongeza kuwa, mikopo iliyotolewa kuanzia mwaka 2021 ni
shilingi milioni 423 taslimu. Wanawake walipata mkopo wa shilingi milioni 203
na vijana shilingi 220 ambapo marajesho mpaka sasa ni milioni 277.7.
Alisema kuwa licha ya kuwepo kwa muitikio mkubwa wa
vikundi hivyo, kumekuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya wanufaika kutorejesha
mikopo hiyo na kuhamia maeneo mengine bila kutoa taarifa. “Changamoto ni kwamba
vikundi vingi vinavyojisajili katika Kata ya Uhuru ni vya wafanyabiashara na
kuna wakati baadhi yao wanafunga biashara na kuondoka bila kutoa taarifa na
baada ya hapo hatujui ni wapi pa kuwapatia” alisema Zahaze.
Ili kukabiriana na changamoto katika utoaji wa mikopo
hiyo alisema kuwa kamati ya mikopo imejipanga kuhakikisha kila kikundi kinakuwa
na wakazi wa kata hiyo wasiopungua wawili ili iwe rahisi kuwapata wanufaika.
Aidha, alieleza kuwa wanatumia njia mbalimbali ikiwemo
mikutano ya wananchi katika kila mtaa na kuzunguka katika mikusanyiko ya watu
wengi ili kuelimisha jamii kuhusiana na suala la mikopo kwa vikundi maalum. “Sisi
tunatoa elimu inayohusu suala la mikopo kwa vikundi maalum kwa kupita kwenye
mikutano ya wananchi inayofanyika ndani ya mitaa yetu. Pia tunazunguka kwenye
maegesho ya bodaboda na vikundi vya mama lishe kutoa elimu” alieleza.
Comments
Post a Comment