Miundombinu S/M Uhuru chachu ya elimu bora
Na. Aisha Ibrahim, UHURU
Diwani wa Kata ya Uhuru, Halfan Kabwe, ameishukuru
serikali ya awamu ya sita chini ya utawala wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa
juhudi kubwa ya kukuza sekta ya elimu kwa maendeleo ya Jiji la Dodoma na taifa
kwa ujumla.
Alitoa shukrani hizo wakati akitoa ufafanuzi wa pesa alizopokea katika kata yake kwaajili ya kukamilisha ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Uhuru, uliogharimu shilingi milioni 76.
Akitoa ufafanuzi wa kina kuhusu ukamilifu wa vyumba vya
madarasa alisema, “kupitia serikali ya awamu ya sita chini ya Rais, Dkt. Samia
Suluhu Hassan, alitupatia kiasi cha shilingi milioni 50 ambazo tuliweza kujenga
madarasa 10 na baadae akatuongeza kiasi cha shilingi milioni 26 zilizotuwezesha
kukamilisha ujenzi wa madarasa hayo” alisema Diwani Kabwe.
Katika hatua nyingine, alimpongeza mbunge kwa kuwa na
moyo wa kujitolea kufuatia ujenzi wa uzio katika shule hiyo kwalengo la
kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora kupitia mazingira rafiki. “Nichukue
fursa hii kumpongeza Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Mheshimiwa Anthony
Mavunde, kwa kutusaidia kujenga uzio wa shule hii kwa kutumia fedha zake
mwenyewe ambapo kabla ya hapo kulikuwa na changamoto kwa wanafunzi kwasababu
sehemu kubwa ya shule hii ilikuwa imevamiwa na magari ya mizigo” alisema.
Pia, aliahidi kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya
elimu ikiwemo kutunza miundombinu ya shule hiyo na kupandisha ufaulu wa
wanafunzi kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla. “Tunaahidi kufanya makubwa katika
sekta ya elimu ikiwemo kutunza miundombinu ya shule hii na kuhakikisha
wanafunzi wanafaulu kwa kiwango cha juu kwasababu Dkt. Samia Suluhu Hassan
anatudai deni kubwa sana kupitia uwekezaji huu” aliongeza Diwani Kabwe.
Kwa upande wake, Mwl. Sospeter Ramadhan, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Uhuru, alieleza kuwa kabla ya kujengwa kwa uzio wa shule hiyo kulikuwa na changamoto kwa wanafunzi katika suala ya nidhamu na taaluma. Sababu kubwa mazingira hayo yamezungukwa na wafanyabiashara wengi waliokuwa wanasababisha muingiliano na wanafunzi jambo linalopelekea washindwe kujifunza kwa utulivu.
Sambamba na hayo, mwanafunzi kutoka shule ya Msingi
Uhuru, Fathiya Saleh, alieleza kuwa kabla ya kujengwa uzio walikuwa wanakutana
na vishawishi mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara wa eneo hilo. Pia vitisho
kutoka kwa walevi na vichaa wanaoingia
eneo la shule jambo lililokuwa linapelekea kukosa amani wawapo shuleni hasa
kipindi cha mapumziko.
Nae, Ikram Mohamed, mwanafunzi kutoka shule hiyo,
aliishukuru serikali kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa na uzio kwasababu kabla
ya hapo walikuwa wanashindwa kukaa darasani na kusoma kwa utulivu. Pia aliahidi
kusoma kwa bidii ili kuunga juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dkt. Samia Suluhu Hassan.
MWISHO
Comments
Post a Comment