Wazazi wapongezwa kuchangia chakula S/M Uhuru
Na. Aisha Ibrahim, UHURU
Wazazi na walezi wamekuwa na mchango mkubwa katika
kupanda kwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi kutokana na juhudi kubwa
wanayoifanya ya kutoa michango na nafaka shuleni ili kuhakikisha wanafunzi
wanapata lishe bora na kuongeza kiwango cha umakini jambo linalopelekea kupanda
kwa kiwango cha ufaulu.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwl. Sospeter Ramadhan, kutoka Shule ya Msingi Uhuru wakati akifafanua kuhusu utekelezaji wa ajenda ya lishe shuleni na umuhimu wake kwa waandishi wa habari waliotembelea shule yake kuona utekelezaji wa agenda ya lishe.
Alisema kuwa katika kuhakikisha wanafunzi wanasoma na
kuelewa, shule hiyo imekuwa na ushirikiano wa hali ya juu na wazazi na walezi
kutoa michango ya fedha na nafaka ili watoto wapate chakula, pia mchango wa
mawazo kwa lengo la kuboresha kiwango cha elimu bora. “Wazazi na walezi
wamekuwa mstari wa mbele kujitolea michango ya fedha na hata mawazo ili
kuhakikisha watoto hawa wanapata chakula wawapo shuleni. Jambo hili ni hamasa
kubwa na hupelekea wanafunzi wetu kufaulu vizuri. Watoto wetu wanapata lishe
kama ifuatavyo; darasa la kwanza na la pili kwakuwa wanarudi nyumbani kwao
ifikapo saa tano asubuhi wao wanapata uji wa lishe pekee. Kuanzia darasa la
tatu mpaka la saba, kwakuwa wanatoka shule saa 10 jioni wao wanapata uji pamoja
na chakula cha mchana” alisema Mwl. Ramadhan.
Kwa upande wake mwanafunzi wa darasa la sita shuleni
hapo, Fathiya Saleh alisema kuwa kabla ya kuletewa mpango wa chakula shuleni,
wanafunzi walikuwa wanashindwa kumsikiliza mwalimu vizuri pindi anapofundisha. “Kabla
hatujaanza kupikiwa shuleni tulikuwa tukikaa darasani mchana tunaanza kusinzia
kwasababu ya njaa na kushindwa kumsikiliza mwalimu akiwa anafundisha” alisema
Saleh.
Aliongeza kuwa, anaishukuru serikali ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia huduma ya chakula shuleni kwasababu kupitia mpango huo umeweza kuinua ufaulu wao kwa kiwango cha hali ya juu na pia aliahidi kusoma kwa bidii na kuweza kufaulu masomo vizuri.
MWISHO
Comments
Post a Comment