Bonanza la Michezo lahamasisha Wananchi kuboresha taarifa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Jiji la Dodoma

Na. Nancy Kivuyo, UHURU

Halmashauri ya Jiji la Dodoma yafanya bonanza la michezo la hamasa kuelekea Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura awamu ya pili kwa lengo la kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha ili wapate haki ya kupiga kura ifikapo mwezi Oktoba, 2025.



Hayo yalisemwa na Afisa Mwandikishaji Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro kabla ya ufunguzi wa bonanza la hamasa kuelekea Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika uwanja wa michezo wa Mtekelezo katika Kata ya Uhuru, jijini Dodoma.

Alisema kuwa lengo la bonanza hilo ni kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwenda kujiandikisha ili wapate fursa ya kupiga kura. “Tunategemea kufanya maboresho ya uandikishaji katika Daftari la Kudumu la Mpiga Kura ili watu wapate sifa ya kupiga kura hapo mwezi Oktoba, 2025. Halmashauri ya Jiji la Dodoma ina vituo 105 na uandikishaji unategemewa kuanza mnamo tarehe 16 – 22 Mei, 2025” alisema Kimaro.

Aliongeza kuwa vituo vitakuwa wazi kuanzia saa mbili asubuhi na kufungwa saa kumi na mbili jioni na wanatilia mkazo hamasa kuwa wananchi wenye sifa wajitokeze. “Wapiga kura wapya ambao wametimiza miaka 18 na wale ambao hadi mwezi Oktoba, 2025 watakuwa wamefikisha miaka 18 wanaruhusiwa kujiandikisha. Hata wale ambao hawakuwahi kujiandikisha nao wanapaswa kujiandikisha na wale wanaohuisha taarifa zao za makazi kutoka eneo moja na wamehamia eneo jingine wanapaswa kwenda kubadili taarifa zao ili wapate haki yao ya msingi ya kupiga kura” aliongeza Kimaro.

Katika hatua nyingine alihimiza vijana wenye sifa kujitokeza ili wapate haki yao ya msingi ya kupiga kura ili kuchagua viongozi bora. “Katika bonanza hili mnajionea wenyewe kundi kubwa lililopo hapa ni vijana, wameonesha mwitikio mkubwa na hawa tunatamani sana wapate hamasa hii ili wakajiandikishe na hatimaye waweze kushiriki katika upigaji kura” alihimiza Kimaro.

Naye mwananchi wa mtaa wa kati, Kata ya Uhuru, Hamida Kapela alisema kuwa amejiandikisha katika awamu ya kwanza kwasababu anatambua umuhimu wa kupiga kura. “Mimi nimejiandikisha tangu mwanzo wa zoezi, nimekitunza kitambulisho changu na nimatumaini mwezi Oktoba, 2025 nitapiga kura kumchagua kiongozi bora atakeendeleza mazuri ambayo serikali inatufanyia” alisema Kapela.

Alihimiza wananchi wa Kata ya Uhuru na Jiji zima la Dodoma hasa wale ambao hawakujishughulisha na zoezi la uandikishaji kujitokeza kujiandikisha ili wapate nafasi ya kupiga kura muda utakapofika. “Nawasisitiza wananchi wenzangu, akina mama, vijana na wale wote wenye vigezo vya kupata kadi ya mpiga kura nendeni mkajiandikishe ili mpate haki yenu ya kikatiba ya kupiga kura na kumchagua kiongozi bora unayemtaka” alihimiza Kapela.

Kwa upande wake Afisa Mwandikishaji Msaidizi ngazi Kata, Kata ya Uhuru, Fatuma Amri alieleza kuwa zoezi la uhamasishaji awamu ya pili linafanyika ili kuwasaidia wale ambao hawakujiandikisha wajitokeze wakajiandikishe. “Katika kata yangu, wananchi wengi ni wafanyabiashara na muda mwingi wanakosa muda wa kutoka lakini nawahimiza kuwa waende wakajiandikishe ili baadaye waweze kupiga kura na kuchagua viongozi wao. Nawahimiza pia vijana wa bodaboda nao wasibaki nyuma mkajiandikishe ili mwezi Oktoba mpige kura ili mpate viongozi watakaoleta maendeleo” alieleza Amri.

Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura linatarajiwa kufunguliwa kuanzia tarehe 16-22 Mei, 2025 katika Halmashauri ya Jiji Dodoma na linatarajiwa kuwa na vituo 105 vitakavyofunguliwa kuanzia saa mbili asubuhi na kufungwa saa kumi na mbili jioni.

MWISHO

 

Comments

Popular Posts

Osterbay Dodoma wajitokeza usafi wa mazingira

Usafi wa Mazingira Kipaumbele Kata ya Chamwino

Wananchi wa Kata ya Mtumba wanufaika na Mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri