Uwanja wa Michezo Kilimani utumike kuboresha Afya za wananchi
Na. Nancy Kivuyo, KILIMANI
Diwani
wa Kata ya Kilimani, Neema Mwaluko amesema suala la michezo katika kata yake
linapewa kipaumbele kupitia hamasa ya ugawaji wa jezi na mipira pamoja na kuhimiza
wananchi kupenda michezo ili kulinda afya zao.
Aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea Kata ya Kilimani kuona shughuli za michezo zinavyofanyika. “Sisi Kata ya Kilimani tunahamasisha sana vijana wetu na watu mbalimbali kushiriki michezo kwasababu tunatambua michezo ni ajira lakini pia michezo ni afya. Bonanza na michezo mingi imekuwa ikifanyika katika uwanja wetu hali inayoonesha ni namna gani kata yetu ni kielelezo bora katika kuhamasisha michezo” alisema Diwani Mwaluko.
Aliongeza
kuwa vijana wa katani hapo wamekuwa wakipewa jezi na mipira ili kuongeza hamasa
ya kufanya mazoezi na kushiriki mashindano mbalimbali. “Jambo hili nimeweza
kulisimamia kwa vitendo, kunapokuwa na changamoto ya vifaa nimekuwa nikiwapatia
jezi pamoja na mipira ili waendeleze vipaji vyao. Malengo yetu ni kuhakikisha
Kata ya Kilimani inaendelea kuwa chachu ya ubora kimichezo katika Jiji la
Dodoma” aliongeza Diwani Mwaluko.
Naye
Afisa Mtendaji wa Kata ya Kilimani, Eliada Msuta alisema kuwa kata hiyo ina
uwanja mzuri wa michezo ambao kuna wakati unatumika kwaajili ya mazoezi na timu
kubwa ikiwemo timu ya mpira wa miguu ya Dodoma Jiji inayoshiriki ligi kuu
Tanzania bara. “Kata yetu ina mwamko mkubwa sana katika masuala ya michezo,
kumekuwa na mashindano mbalimbali yakifanyika hapo na wananchi wanaburudika
kutumia uwanja huo” alisema Msuta.
Kwa upande mwingine mwananchi wa Kata ya Kilimani, Jonas Masanika alieleza kuwa hamasa ya kushiriki katika michezo wanayopata kutoka kwa viongozi wao wa kata inawasaidia katika kuimarisha afya. “Tunawashukuru sana viongozi wetu kwa kuendelea kutuhamasisha kupenda michezo na kwakweli kuna mwamko mkubwa sana. Tunatambua michezo ni ajira lakini pia inaboresha afya na kustawisha umoja na mshikamano tunapokutana mara kwa mara, napenda kuwahimiza wananchi wenzangu kupenda michezo” alishukuru Masanika.
MWISHO
Comments
Post a Comment