Utunzaji Mazingira Kata ya Kilimani kielelezo bora cha kuigwa
Na. Nancy Kivuyo, KILIMANI
Kata
ya Kilimani yaendelea kuhimiza kwa vitendo utunzaji wa mazingira kwa kupanda
miti mbalimbali ikiwemo ya kivuli pamoja na matunda ili kuweka mazingira safi
na ya kuvutia jambo linalowafanya wananchi wake kufurahia mandhari na kuwa na
lishe bora.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kata hiyo kujionea utunzaji wa mazingira unavyofanyika Diwani wa Kata ya Kilimani, Neema Mwaluko alisema kuwa wanajitahidi kupanda miti ili kuweka mazingira katika hali nzuri inayovutia. “Sisi hapa Kilimani tuna program za kupanda miti kila mwaka. Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kila mwaka inatupatia miche ya miti kwaajili ya kupanda katika kata yetu” alisema Diwani Mwaluko.
Aliongeza
kuwa wanatoa elimu ya utunzaji mazingira kwa wananchi wa kata hiyo ili
kuhakikisha wanakuwa vinara na mfano wa kuigwa katika Jiji la Dodoma. “Kwa
ujumla kata yetu inafanya vema katika utunzaji wa mazingira. Kama mnavyojionea
sehemu kubwa ni kijani, kila kaya unayoona ina miti na mazingira yanavutia.
Tutaendelea kuwaelimisha wananchi kutunza mazingira ili yatufae sote na vizazi
vijavyo” aliongeza Diwani Mwaluko.
Naye
mwananchi wa Kata ya Kilimani, Jonasi Masanika alisema kuwa wamenufaika na
uongozi uliopo kwasababu unawahamasisha kutunza mazingira. “Kipekee niwashukuru
viongozi wa kata, wanatuelimisha na kutuhamasisha kupanda miti na kutunza
mazingira. Vijana tunahusika sana katika kupokea elimu hiyo na tunaishukuru
sana serikali kwa kutubeba hata katika masuala kama haya” alishukuru Masanika.
Kata
ya Kilimani ni miongoni mwa kata 41 zilizopo katika Halmashauri ya Jiji la
Dodoma. Kata hiyo ina jumla ya wakazi 9,562 ambapo wanaume ni 4,609 na wanawake
ni 4953. Shughuli zinazofanyika ni kilimo na ufugaji na shughuli za kiuchumi ni
biashara za jumla na rejareja na ujasiriamali.
MWISHO
Comments
Post a Comment