Shule mpya ya Msingi Chinyoyo ya kwanza kujengwa Kata ya Kilimani
Na. Emmanuel Charles, KILIMANI
Mradi wa ujenzi wa shule
mpya ya Chinyoyo, Kata ya Kilimani unaogharimu shilingi 147,000,000 ni shule ya
kwanza kujengwa katani hapo na itaondoa adha ya wanafunzi ya kutembea umbali
mrefu kufuata masomo.
Haya yalisemwa na Diwani wa
Kata ya Kilimani, Neema Mwaluko wakati akizungumza na waandishi wa habari
waliofanya ‘Media Tour’ kukagua miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali
kuanzia 2021-2025 katika kata hiyo.
Alisema kuwa kwasababu kata
yake ipo mjini, miundombinu ikiwemo ya elimu ilichelewa kufika na sasa serikali
ya awamu ya sita inajenga shule ya msingi ili kuwakwamua watoto wanaotembea
umbali mrefu. “Kwa miaka yote ya nyuma, kata hii haikuwahi kuwa na shule yeyote
na wanafunzi wanalazimika kutembea umbali mrefu kufuata masomo katika kata za jirani.
Tunaishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kutuona na kuamua kutenga eneo la
kujenga Shule ya Msingi Chinyoyo kwa gharama ya shilingi 147,000,000 ambapo
ujenzi wa madarasa manne na ofisi mbili umegharimu shilingi 110,000,000, matundu
10 ya vyoo shilingi 17,000,000 na uchimbaji wa kisima shilingi 20,000,000. Shule
hii itakapokamilika tunaamini itakuwa mkombozi kwa wanafunzi wa kata hii hasa
wale wadogo hawatatembea tena kwenda mbali” alisema Diwani Mwaluko.
Aliongeza kuwa ujenzi wa
mradi huo utapunguza adha nyingi zilizokuwa zinawakabili watoto na kuwapa
nafasi ya kufurahia upatikanaji wa elimu bora katika shule hiyo. “Watoto wa
kata hii walikua wanakumbwa na adha nyingi sana ikiwemo utoro na kutokuwepo
usalama wa watoto wanapokuwa wanatembea wenyewe. Niwahakikishie wananchi kuwa
uwepo wa shule hii utawasaidia watoto kusoma vizuri na hizo changamoto
zilizokuwepo mwanzoni zitapungua na hatimaye kuisha kabisa. Tunamshukuru
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kwa upendeleo huu na kiwanja cha eneo hili la
shule kimeshapimwa. Hivyo, tutasimamia mradi huu ukamilike kwa wakati ili
watoto waanze masomo mara moja” aliongeza Diwani Mwaluko.
Kwa upande mwingine Diwani
Mwaluko alisema kuwa katika eneo hilo yapo maeneo yameshapimwa kwaajili ya
ujenzi wa shule ya sekondari, kituo cha polisi na kituo cha afya ambapo
miundombinu hiyo itasaidia kwa uteshelevu mahitaji ya wakazi wa Kilimani.
Naye Afisa Mtendaji wa Mtaa
Chinyoyo, Happyness Japhet alieleza kuwa serikali ya awamu ya sita imefanya
vizuri sana kujenga shule hiyo kwasababu itawasaidia wanafunzi kusoma karibu na
kupata elimu bora. “Serikali yetu ni sikivu imeweza kusikiliza kilio cha
wananchi na kujenga shule hii. Watoto wadogo wa shule ya awali walikua
wanataseka kuamka alfajiri na kutembea umbali mrefu kufuata shule. Shule hii ni
mkombozi wa wananchi wa Chinyoyo na changamoto zote zitabaki historia. Hongera
nyingi kwa serikali yetu sikivu” alieleza Japhet.
MWISHO
Comments
Post a Comment