WAKAZI WA NALA WAADHIMISHA MIAKA 62 YA MUUNGANO KWA KUSHIRIKI USAFI WA MAZINGIRA
Na. Mwandishi Wetu, NALA - DODOMA
WAKAZI
wa Mtaa wa Barazani, Kata ya Nala wamejitokeza kwa wingi katika zoezi la usafi
wa mazingira linalofanyika kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kwa lengo la
kuendelea kuhakikisha mji unakuwa safi na kujenga mazoea ya kupenda kufanya
usafi.
Zoezi
hilo la usafi limekuwa la kipekee kwasababu limefanyika sambamba na kuadhimisha
Miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambapo wananchi walionekana
wenye hamasa kubwa katika kuboresha muonekano wa mtaa wao.
Akizungumza
na wakazi ho mara baada ya zoezi la usafi kukamilika, Afisa Mazingira kutoka
Kanda Namba Tatu, Neema Komba aliwapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na
kuonesha uthamani wa kuishi katika mazingira safi. “Leo tumefanya jambo jema
sana kujitokeza kufanya usafi, kwanza tumetimiza ule wajibu wetu wa kufanya
usafi kila jumamosi ya mwisho wa mwezi lakini pia tupo hapa kuadhimisha kwa
umoja wetu miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Muungano huo
unaendelea kutukumbusha kushirikiana na kusaidiana ili nchi yetu iendelee kuwa
na amani. Ushiriki huu ni ishara ya ukomavu wa kijamii na uwajibikaji katika
kutunza afya za wakazi wa Nala” alisema Komba.
Aidha,
Aliwahimiza wananchi kuendeleza utamaduni wa kufanya usafi kila wakati ili
kuepuka magonjwa ya mlipuko yanayotokana na uchafu. Alisisitiza kuwa mazingira
bora ni msingi wa afya imara na kila mwananchi anapaswa kuwa mlinzi wa mwenzake
kwa kuhakikisha maeneo yanayowazunguka yanabaki kuwa salama na safi.
Nae,
Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Nala, Alinikisia Humbo alisema kuwa usafi wa
mazingira unapaswa kufanyika bila shuruti ili kuepuka taka zinazozagaa hovyo
katika mitaa ambazo ni hatari kwa afya za wakazi. “Naomba kuwakumbusha kuwa
usafi wa mazingira ni suala muhimu sana. Mmejionea taka zilizokuwa zimezagaa
hapa, tusaidiane katika kukemea wale wanaotupa taka bila utaratibu ili
tuwadhibiti kwasababu ndio wanafanya taswira ya jiji letu kuonekana chafu.
Ifike mahala tuone aibu kutupa taka hovyo, tuyatunze mazingira ili nayo
yatutunze na vizazi vijavyo” alisema Humbo.
Zoezi
hilo la usafi wa mazingira lilikuwa mahsusi kwa ajili ya kuuenzi Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar ambao unatarajiwa kuadhimishwa tarehe 26 Aprili, 2026
ukiwa na kaulimbiu isemayo “Miaka 62 ya Muungano: Amani, Umoja na Mshikamano ni
Msingi wa Maendeleo Endelevu.
MWISHO
Comments
Post a Comment