OFISI ZA KANDA ZASOGEZA HUDUMA KWA WANANCHI DODOMA

Na. Mwandishi Wetu, DODOMA

Jiji la Dodoma lilianzisha Kanda Saba kwaajili ya kusogeza huduma kwa wananchi lakini lengo kuu likiwa ni kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri ambayo yanatumika katika kuleta maendeleo kwa jamii.



Akizungumza katika Mkutano wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma la kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa kazi zilifanyika kwa kipindi cha robo ya tatu, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Alimwoni Chaula alisisitiza umuhimu wa matumizi ya mfumo wa kanda katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kubuni vyanzo vipya na kuviimarisha vilivyopo.

Alisema kuwa mfumo wa kanda umeendelea kutoa mafanikio makubwa kwa kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato, kuimarisha usimamizi wa vyanzo vya mapato na kuongeza uwajibikaji kwa wataalam waliopo katika maeneo husika.

"Katika kipindi cha robo ya tatu, matumizi ya mfumo wa kanda yamesaidia kuongeza ufuatiliaji wa karibu wa vyanzo vya mapato ikiwemo ushuru, leseni za biashara, ada mbalimbali, mapato ya masoko, stendi, mabango pamoja na mapato yatokanayo na huduma.

“Mfumo wa kanda umeongeza uwajibikaji na usimamizi wa mapato kwa ukaribu zaidi. Kila kanda imekuwa na nafasi ya kutambua changamoto zake na kuzitatua kwa wakati ili kuongeza makusanyo,” alisema Chaula.

Aidha, alieleza kuwa mafanikio hayo yamechangia kuongeza uwezo wa halmashauri katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi. Aliitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi na ukarabati wa barabara, miradi ya elimu, afya, pamoja na usafi wa mazingira.



Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Ihumwa, Edward Magawa alitoa pongezi kwa uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuendelea kusimamia kwa karibu ukusanyaji wa mapato, wakieleza kuwa mfumo wa kanda umeongeza uwazi na uwajibikaji katika halmashauri.

"Kanda hizi zimetusaidia, ila nishauri kuwa mameneja wote wakae na viongozi wa kanda, kata na mitaa kwaajili ya kujadili namna nzuri ya kuongeza mapato. Pia kubuni vyanzo vingine ambayo vitaisaidia halmashauri kupata mapato," alisema Magawa.

MWISHO

Comments