KANDA NAMBA MBILI YAADHIMISHA MIAKA 62 YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR KWA KUFANYA USAFI WA JUMAMAMOSI YA MWISHO WA MWEZI
Na. Tutindaga Nkwindi, DODOMA
KANDA Namba Mbili imeadhimisha miaka 62 ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar kwa kufanya zoezi la usafi katika Kata ya Nzuguni, Mtaa
wa Nzuguni A pamoja na Kituo Kikuu cha Mabasi Dodoma ikiwa ni sehemu ya kuenzi
umoja na mshikamano wa watanzania.
Zoezi hilo liliongozwa na Meneja wa Kanda Namba Mbili,
Hussen Nyenye aliyeshirikiana na watumishi wa kanda hiyo pamoja na wananchi
kusafisha mazingira katika maeneo hayo muhimu ya jiji.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo aliwashukuru Kikundi cha
Wanawake wa Stendi maarufu kama Malkia wa Nguvu kwa kujitokeza kwa wingi
kushiriki usafi huo. “Nawapongeza sana Malkia wa Nguvu kwa kuungana nasi
kusafisha eneo hili muhimu ikiwa ni moja ya njia za kuadhimisha muungano wetu
huku tukizingatia kaulimbiu ya mwaka huu isemayo ‘Miaka 62 ya Muungano: Amani,
Umoja na Mshikamano ni Msingi wa Maendeleo Endelevu'. Pia tukumbuke kuwa
mazingira safi ndiyo msingi wa kila kitu katika maendeleo ya jamii” alisema
Nyenye.
Kwa upande wake, mwanachama wa Kikundi cha Malkia wa nguvu
Subira Mtandi alisema kuwa wanawake wanaofanya kazi katika Kituo Kikuu cha
Mabasi Dodoma wameona umuhimu wa kuuenzi muungano kwa vitendo. “Sisi wanawake
tunaofanya kazi hapa stendi, tumeamua kuuenzi muungano wetu kwa kufanya usafi
katika eneo letu la kazi ili kudumisha mazingira bora” alisema Mtandi.
Nae, Afisa Mazingira wa Kanda Namba Mbili, Neema Mbawala
aliwashukuru wakazi wa Mtaa wa Nzuguni A kwa kujitokeza kushiriki zoezi la
usafi, akieleza kuwa usafi ni njia mojawapo ya kuimarisha mshikamano na
kuadhimisha muungano kwa vitendo.
Maadhimisho hayo yameonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya
viongozi na wananchi katika kulinda mazingira, huku yakisisitiza kuwa amani,
umoja na mshikamano vinabaki kuwa nguzo kuu ya maendeleo endelevu ya taifa.
MWISHO
Comments
Post a Comment