Jiji la Dodoma laaga Timu ya Watumishi kuelekea SHIMISEMITA Mbeya

Na. Rahma Magona, DODOMA

Uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma umeiaga rasmi timu ya watumishi itakayoiwakilisha Halmashauri hiyo katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Serikali za Mitaa Tanzania (SHIMISEMITA), yanayotarajiwa kufanyika jijjni Mbeya.



Hafla hiyo ya kuwaaga watumishi hao ilifanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, ambapo watumishi hao wamepewa jukumu la kuiwakilisha Dodoma katika mashindano hayo na kurudi na ushindi.


Akizungumza katika hafla hiyo Kocha wa Timu ya Mpira wa Miguu, Leonard Mkinga alisema kuwa kabla ya kuingia kwenye mashindano, watumishi wamejiandaa vizuri katika kipindi chote kwa kufanya mazoezi ya viwango vya juu. “Tumejiandaa vizuri na matarajio yetu lazima tukaoneshe ushindani wa hali ya juu na kutetea vikombe tulivyovipata mwaka jana” alisema Mkinga.

 

Alisema kuwa ushiriki wa watumishi hao katika michezo unapaswa kwenda sambamba na utekelezaji wa majukumu yao ya msingi ya utumishi, huku michezo ikiwa na nafasi muhimu katika kuimarisha afya, kujenga mahusiano mazuri na utekelezaji wa majukumu ya kila siku.


Kwa upande wake Mchezaji wa Mpira wa Miguu, Ramadhan Nassor alisema kuwa michezo inawapa watumishi nafasi ya kujuana zaidi, kusaidiana na kujenga hali ya kufanya kazi kwa pamoja kama timu, jambo linalosaidia kuimarisha ushirikiano wao katika kutekeleza majukumu ya kila siku.

Ushiriki wa timu hiyo jijini Mbeya unaonesha jitihada za Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika kuhamasisha watumishi kushiriki katika michezo, huku wakitambua umuhimu wa afya, umoja na ushirikiano katika mazingira ya kazi.

Comments

Popular Posts

Timu ya Watumishi Jiji la Dodoma inayoshiriki SHIMISEMITA yatakiwa kurejea na ushindi

Dodoma Jiji yajiandaa Ngoma na Kwaya SHIMISEMITA, 2026

Timu ya Watumishi Jiji la Dodoma waagwa kuelekea SHIMISEMITA