KAMATI YA KUDHIBITI UKIMWI KUTOA ELIMU YA KINGA KWA VIJANA DODOMA

Na. Mwandishi Wetu, DODOMA

Kamati ya Kuzuia na Kudhibiti UKIMWI ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kushirikiana na Taasisi ya DOYODO imeendelea kutoa elimu na mafunzo kwa jamii, hususan kwa vijana, ili kuhakikisha wanapata uelewa sahihi wa namna ya kujikinga na ugonjwa huo.


Hayo aliyasema Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Dodoma (WASEMI), Leticia Sanga tarehe 29 Aprili, 2026 wakati alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kudhibiti UKIMWI kwa kipindi cha robo ya tatu kuanzia Januari hadi Machi, 2026 katika Mkutano wa Baraza la Madiwani uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Alisema kuwa juhudi hizo zimeanza kuzaa matunda, lakini bado kuna haja ya kupanua wigo wa elimu hiyo. “Tumekuwa tukiwalenga zaidi vijana, lakini sasa tumeona umuhimu wa kuwafikia pia wazee. Wazee wengi wamekuwa waathirika wakubwa wa janga hili kwa sababu wanabeba jukumu la kuwahudumia watoto wao wanaoishi na virusi vya UKIMWI. Hivyo, nao wanahitaji elimu hii kwa kina zaidi” alisema Sanga.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Chahwa, Jorome Petro alisisitiza umuhimu wa kupeleka elimu hiyo katika maeneo ya pembezoni mwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, akieleza kuwa bado kuna upungufu mkubwa wa uelewa katika maeneo hayo.

“Elimu hii isiishie katikati ya jiji pekee. Tuendelee kuwafikia wananchi wa kata za pembezoni ambao mara nyingi hukosa taarifa sahihi na hivyo kubaki nyuma katika mapambano haya. Hivyo, naomba elimu hii iwafikie na waliopo pembezoni mwa mji” alisema Petro.

Naye Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Alimwoni Chaula, alitoa wito kwa wadau wote kutumia vema fursa ya Mbio za Mwenge wa Uhuru kueneza elimu dhidi ya mapambano ya UKIMWI kwa jamii kupitia vyombo vya habari.

“Tunapoelekea kwenye Mbio za Mwenge wa Uhuru tutumie nafasi hii katika kutoa elimu kwa dhamira ya kutumia kila jukwaa, hususan vyombo vya habari, kuelimisha jamii kuhusu namna ya kujikinga na UKIMWI. Elimu ndiyo silaha kuu ya kumaliza janga hili” alisema Chaula.

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma lilisisitiza ushirikiano wa wadau mbalimbali na utoaji endelevu wa elimu kwa makundi yote ya jamii ni msingi muhimu katika kufikia lengo la kutokomeza UKIMWI nchini.






MWISHO

Comments

Popular Posts

Juhudi na nidhamu yatakiwa kwa washiriki wa mafunzo ya Jeshi la Akiba Dodoma

Wanafunzi Dodoma watakiwa kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia