DODOMA YAADHIMISHA MIAKA 62 YA MUUNGANO, DC SHEKIMWERI ASISITIZA AMANI NA MSHIKAMANO

Na. Tutindaga Nkwindi, DODOMA

MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Mhe Alhaji Jabir Mussa Shekimweri, ameongoza kilele cha maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika kimkoa katika Shule ya Msingi Nane Nane, Kata ya Nzuguni, akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, umoja na mshikamano ili kuchochea maendeleo endelevu ya Taifa.


Akizungumza katika maadhimisho hayo, Alhaj Shekimweri alisema kuwa kaulimbiu ya mwaka huu isemayo “Miaka 62 ya Muungano: Amani, Umoja na Mshikamano ni Msingi wa Maendeleo Endelevu” inapaswa kila Mtanzania aiishi kwa vitendo.

Alieleza kuwa mafanikio ya taifa yanategemea mshikamano wa wananchi wake, akisisitiza umuhimu wa kulinda amani na kufanya kazi kwa pamoja ili kufikia maendeleo ya kweli na ya kudumu. “Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuilinda amani, kuimarisha umoja na mshikamano kwasababu hayo ndiyo msingi wa maendeleo endelevu ya nchi yetu. Aidha, tujishughulishe na shughuli za kiuchumi ili kujikwamua na kuinua hali zetu za maisha” alisema Alhaj Shekimweri.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Dodoma, Sakina Mbugi alisema kuwa maadhimisho hayo yalianza tangu tarehe 24 Aprili, 2026 yakihusisha shughuli mbalimbali za kijamii na maendeleo.

Alifafanua kuwa wilaya ilifanya usafi wa mazingira katika kata zote, matembezi ya amani, bonanza la michezo na kongamano kupitia vyombo vya habari huku washindi wakitarajiwa kupokea zawadi katika kilele hicho. “Tumehitimisha maadhimisho haya kwa kupanda miti 162 ambapo mti mmoja unaashiria taifa moja lenye amani na mshikamano, na miti 62 inaakisi miaka ya muungano tangu kuanzishwa kwake” alisema Mbugi.

Maadhimisho hayo yameweka msisitizo mpya kwa wananchi wa Dodoma kwa ujumla juu ya umuhimu wa kuenzi na kulinda tunu za muungano kwa vitendo, huku yakihamasisha ushiriki wa pamoja katika kujenga uchumi imara na kufikia maendeleo endelevu.




MWISHO

Comments