Watoto 328 wenye mahitaji maalum wabainishwa Jiji la Dodoma
Na. Mwandishi wetu, DODOMA
Afisa Elimu Maalum Jiji la
Dodoma, Mwl. Issa Kambi, amekabidhi rasmi taarifa ya zoezi la ubainishaji wa
watoto wenye mahitaji maalum kwa Kaimu Mkurugenzi wa Jiji hilo, Dkt. Pima
Sebastian, katika hatua muhimu ya kuimarisha huduma za elimu jumuishi.
Zoezi hilo la ubainishaji lililofanyika katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma limepata watoto 328 ambao wamebainishwa ikiwa na lengo la kutambua watoto wenye mahitaji maalum, wakiwemo wenye ulemavu wa aina tofauti pamoja na changamoto za kujifunza ili waweze kupatiwa msaada stahiki wa kielimu na kijamii.
Akikabidhi taarifa hiyo,
Mwl. Kambi alieleza kuwa matokeo yanaonesha uwepo wa idadi kubwa ya watoto
wanaohitaji uangalizi na mipango maalum ili waweze kunufaika kikamilifu na haki
yao ya kupata elimu.
Aidha, alisisitiza umuhimu
wa ushirikiano kati ya wazazi, walimu, wataalamu wa afya pamoja na wadau
wengine wa maendeleo katika kuhakikisha watoto hao wanapatiwa mazingira rafiki
ya kujifunzia.
Aliongeza kuwa takwimu
zilizokusanywa zitasaidia Jiji kupanga mikakati madhubuti ya kuboresha
miundombinu ya shule, kuongeza walimu wa elimu maalum pamoja na upatikanaji wa
vifaa saidizi.
Kwa upande wake, Dkt. Pima Sebastian alipokea taarifa hiyo na kuipongeza timu ya elimu maalum kwa kazi kubwa waliyoifanya.
Aliahidi kuwa Jiji
litatumia taarifa hiyo kama nyenzo muhimu katika kupanga na kutekeleza mipango
ya kuboresha huduma za elimu jumuishi, sambamba na kuhakikisha hakuna mtoto
anayeachwa nyuma.
Hatua hiyo inaonesha dhamira ya Jiji la Dodoma katika kuhakikisha usawa wa fursa za elimu kwa watoto wote, hususan wale wenye mahitaji maalum na kuendelea kujenga jamii inayojali na kujumuisha kila mwananchi.
Comments
Post a Comment