Wamiliki wa Viwanja watakiwa kuvisafisha na kuviendeleza Dodoma
Na. Mwandishi Wetu, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imewataka wananchi na
taasisi kusafisha, kuendeleza na kulinda mipaka ya viwanja vyao na kueleza kuwa
kushindwa kufanya hivyo, vitatolewa kwa watu wengine wenye uhitaji wa viwanja
kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dennis Gondwe alisema
kuwa wananchi na wamiliki wote wa viwanja wana wajibu wa kusafisha viwanja
vyao. “Ndugu waandishi wa habari, Halmashauri ya Jiji la Dodoma inapenda
kuwataarifu wananchi wote pamoja na taasisi ambazo zinamiliki viwanja ndani ya
Jiji la Dodoma kuendeleza viwanja hivyo kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Namba 4
ya Mwaka 1999 (Sura ya 113). Sheria hiyo, inawataka wananchi wote pamoja na
taasisi zinazomiliki viwanja kuviendeleza viwanja hivyo ndani ya muda usiozidi
miezi 36 tangu walipokabidhiwa au kumilikishwa” alisema Gondwe.
Alisema kuwa limeibuka wimbi la watu wasio na nia njema
wanaovamia viwanja ambavyo havijasafishwa, kuendelezwa na kujimilikisha viwanja
hivyo. “Aidha, wananchi wengine wamefikia hatua ya kung’oa ‘beacons’ na
kusababisha usumbufu mkubwa kwa wamiliki wa viwanja hivyo kwa mujibu wa sheria
kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine usumbufu kwa halmashauri ambayo ndiyo
mamlaka ya upangaji, upimaji na umilikishaji. Vilevile, kumekuwa na wimbi la
kuvamia mipaka ya viwanja katika baadhi ya maeneo. Nitumie hadhira hii
kuwataarifu kuwa haya ni makosa kama yalivyo makosa mengine” alisema.
Akitoa kauli rasmi ya halmashauri alisema kuwa kila
mmiliki wa kiwanja anapaswa kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria. “Kwa
Ilani hii, Halmashauri ya Jiji la Dodoma inawataka wananchi wote na taasisi
zote kulinda mipaka ya viwanja vyao, kuendeleza viwanja au maeneo yao kwa
mujibu wa sheria. Kutofanya hivyo, halmashauri itaendelea na taratibu za kufuta
miliki hizo kwa mujibu wa sheria” alisema Gondwe.
MWISHO
Comments
Post a Comment