Prof. Mohamed ahimiza wanafunzi kusoma kwa bidii na kuwapongeza wazazi
Na. Mwandishi Wetu, DODOMA
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Makutupora watakiwa
kuwa na nidhamu na kusoma kwa bidii ili kufikia malengo yao ya kielimu na
maisha kwa ujumla.
Hayo aliyasema Katibu Mtendaji Baraza la Mitihani la Tanzania, Prof. Said Mohamed wakati wa Uzinduzi wa Upandaji Miti mwaka 2025/2026 uliofanyika katika Shule ya Sekondari Makutupora Jijini Dodoma.
Alisema kuwa juhudi za wanafunzi katika masomo ni
msingi muhimu wa maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla. “Msingi mzuri wa
watoto ni kupata elimu hivyo niwasihi wanafunzi muendelee kusoma kwa bidii ili
kuweza kufikia ndoto zenu, kwasababu hapa kuna viongozi wa baadae ambao
wataweza kuongoza taifa letu, lakini pia muwe na nidhamu kwasababu nidhamu ndio
hupelekea kufika mbali hususan katika masomo yenu” alisema Prof. Mohamed.
Aidha aliwapongeza wazazi kwa juhudi wanazozifanya
katika malezi ya watoto. “Nipende kuwapongeza wazazi kwa namna ambavyo
mnaendelea kuwalea watoto katika misingi bora, lakini pia nisisitize
ushirikiano kati ya wazazi pamoja na walimu kwasababu ushirikiano ni nguzo
muhimu katika kufanikisha elimu bora kwa watoto” alisema Prof. Mohamed.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Makutupora,
Mwl. Didas Ndalu alimshukuru Katibu Mtendaji kwa kutembelea shule hiyo akieleza
kuwa ujio wake ni faraja kubwa kwa wanafunzi na walimu. “Ni heshima kubwa kwetu
kumpokea kiongozi huyu muhimu. Tunatarajia kuendelea kuinua kiwango cha taaluma
na kuhakikisha wanafunzi wanapanda daraja mwaka hadi mwaka. Kutokana na walimu
kuendelea kusimamia nidhamu ya wanafunzi ufaulu umeendelea kuongezeka ikiwa kwa
mwaka 2025 shule ilifaulu kwa GPA ya 3.4842, lakini pia tunaendela kuweka
mikakati ya kuhakikisha tunafuta daraja sifuri na nne” alisema Mwl. Ndalu
Nae mzazi alieshiriki katika uzinduzi wa upandaji miti,
Phatina Mbeyu alisema kuwa wazazi wataendelea kushirikiana na walimu katika
kuhakikisha watoto wanalelewa katika maadili mema. “Malezi bora kwa mtoto yanachangia kwa kiasi
kikubwa mafanikio katika masomo yao" alisema Mbeyu
Comments
Post a Comment