Kata ya Mnadani yahimizwa kuzingatia usafi wa Mazingira
Na. Mwandihsi wetu, MNADANI
Diwani wa Kata ya Mnadani, Mugendi Kerenge
amewakumbusha wananchi wa Mtaa wa Mnadani kuzingatia usafi wa mazingira ikiwemo
utoaji wa taka mapema na pia ulipaji wa ada ya taka ambayo ni mapato ya
halmashauri.
Aliyazungumza hayo katika mkutano wa hadhara
uliofanyika katika Mtaa wa Mnadani jijini Dodoma.
Alisema kuwa usafi wa mazingira unafanywa ili kujikinga
na magonjwa pamoja na kuboresha mandhari ya eneo husika. Pia alisisitiza kuwa
usafi wa mazingira ni jukumu la kila mwananchi na si la serikali pekee.
"Ni wajibu wetu sote kuhakikisha mazingira yanakuwa safi wakati wote.
Tukifanya hivyo, tutajikinga na magonjwa ya mlipuko na kuongeza hadhi ya mtaa
wetu, niwatake vikundi vinavyohusika katika uondoshaji wa taka kwenye kata hii
muwe na ratiba ambayo itamjulisha mwanchi ni siku gani mtapita katika mtaa
anaoishi" alisema Kerenge.
Aidha, aliwataka wananchi kuacha tabia ya kutupa taka
hovyo na badala yake kutumia maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya ukusanyaji
wa taka, huku akisisitiza umuhimu wa kushiriki katika shughuli za usafi wa
pamoja. “Nitoe rai kwa wananchi kuwa ada ya taka ni lazima kwahiyo kwa yeyote
asiyetoa atalipishwa faini kulingana na sheria ndogo za mazingira maana baadhi
ya wananchi wamekuwa wakikiuka sheria hizi” alisema Kerenge.
Kwa upande wake Mwananchi wa Mtaa wa Mnadani, Mwadawa
Omari alisema kuwa changamoto ya ukusanyaji wa taka bado ipo katika maeneo yao,
wakiiomba serikali ya mtaa kuboresha huduma hiyo ili kuwezesha mazingira kuwa
safi zaidi.
Alishauri kuwa, wahusika wanaoondosha taka kwenye mitaa
wazingatie ratiba kwasababu taka zikikaa muda mrefu husababisha harufu ambayo
inaleta kero kwa wananchi na wapita njia.
MWISHO
Comments
Post a Comment