Mbunge Mavunde kuwekeza zaidi Sekta ya Elimu
Na. Dennis Gondwe
Mbunge
wa Jimbo la Dodoma mjini, Anthony Mavunde ameahidi kuendelea kuwekeza katika
sekta ya elimu ili kuwawezesha wanafunzi wa Dodoma kusoma vizuri na kufikia
malengo yao.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alipokuwa akitoa salamu za Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini katika mkutano wa wadau wa elimu Wilaya ya Dodoma uliofanyika katika ukumbi wa Shule ya St. Gasper jijini Dodoma.
Alhaj
Shekimweri alisema “Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini anasema kuwa nitaendelea
kuwekeza zaidi kwenye elimu ili kuwasaidia watoto wa Dodoma kufikia malengo
yao. Nitashirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuinua na kuboresha elimu
katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma hasa katika miundombinu na mazingira
rafiki ya kusomea”.
Akiongelea
mapinduzi katika teknolojia, alisema kuwa Dodoma inaelekea kupiga mapinduzi
makubwa kwenye elimu. “Dunia inakwenda kwenye mapinduzi makubwa ya teknolojia, lazima
tutumie maendeleo hayo katika kurahisisha ufundishaji wa wanafunzi. Ni jambo la
msingi sana. Ukifika pale shule ya sekondari Dodoma utaona serikali ya awamu ya
sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Ofisi ya Rais, Tamisemi
na Taasisi ya Elimu Kibaha na wafadhili imewekeza mfumo wa ‘e-learning’ na Shule
ya Sekondari Dodoma ni miongomi mwa shule 10 zinazofanyiwa majaribio. Mwalimu
akiwa Kibaha mkoani Pwani au Dodoma anaweza kuwa darasani kufundisha wanafunzi wa
darasa lake, wanamuona na kufundisha wanafunzi wa shule nyingine na kumuona na
kuuliza maswali na kujibiwa” alisisitiza Alhaj Shekimweri.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Fungo akiongelea mafanikio ya sekta ya elimu |
Awali
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Fungo alisema kuwa
kila mdau wa elimu ana nafasi katika mafanikio ya sekta ya elimu. “Sote tupo
hapa na tunahusika moja kwa moja kuhakikisha watoto wetu wanapata elimu bora.
Hivyo, tutajadili tulipo na jinsi ya kuendelea mbele na namna ya kutatua
changamoto za elimu. Tunajua serikali ya awamu ya sita imefanya mambo makubwa na
kuweka msingi utakaowasaidia watoto wetu na taifa letu kusonga mbele katika
maendeleo na kuboresha huduma za kijamii. Katika kuunga mkono juhudi hizo, leo
tutatoa tuzo kwa walimu waliofanya vizuri katika shule na majukumu yao, lakini
pia wapo wanafunzi ambao wamefanya vizuri katika masomo yao. Hiyo itakuwa
chachu kwa wengine kufanya vizuri zaidi.
MWISHO
Comments
Post a Comment