DC Shekimweri ampa Tano Mkurugenzi John Kayombo
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MKUU wa Wilaya ya Dodoma,
Alhaj Jabir Shekimweri amemshukuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma
kwa kutoa kipaumbele katika maendeleo ya sekta ya elimu kwa kutoa fedha nyingi
katika ujenzi wa miundombinu ya sekta ya elimu.
Alhaj Shekimweri alisema
“nitakuwa nimekosa uungwana nisipomshukuru hadharani Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma, John Lipesi Kayombo. Tulikuwa na mkutano wa viongozi wakuu
wa Wilaya ya Dodoma, Mstahiki Meya, Mbunge, Mkurugenzi wa Jiji na Mwenyekiti wa
Chama cha Mapinduzi mzee Mamba. Akiwa mgeni tukataka tushirikiane nae kwenye
dira ya wilaya na tukataka tufahamu vipaumbele vyake kama kijana ambae anataka
kuacha alama katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Nataka niwaambie leo
hadharani, Kayombo alisema mimi napokea maelekezo na ushauri wenu wote
mnaonipatia kama viongozi wangu, lakini la kwangu lililo moyoni mwangu
ninatamani niache alama katika sekta ya elimu”.
Alisema kuwa mkurugenzi
huyo ametoa fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya elimu. “Lakini leo
kuna kitu cha ‘surprise’ nimekiona hapa, anakwenda kutambua divisheni kwa
jitihada walizozifanya na kuwapatia fedha. Najua ukubwa wa sekta ya elimu
msingi na wingi wa shule na wataalamu wanaosimamia, amewapatia shilingi 5,000,000
kutambua jitihada zao kwa kazi wanazozifanya hiki ni kitu kikubwa sana. Lakini ametoa
shilingi 3,000,000 kwa upande wa elimu sekondari pia kutambua jitihada zao.
Ninaongea na wadau wa elimu na wakuu wa shule na walimu wakuu na waratibu elimu
kata, nina dhani mmepata pacha mzuri wa kufanya nae kazi, hebu mumpatie
ushirikiano mzuri ninaenda kuiona wilaya yetu ikipaa kielimu kwa ajili ya kazi
za huyu mkurugenzi” alisema Alhaj Shekimweri.
MWISHO
Comments
Post a Comment