Jiji la Dodoma kinara taaluma
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeendelea kufanya vizuri
katika taaluma kwa kufaulisha kwa asilimia 93.18 wanafunzi waliohitimu elimu ya
msingi mwaka 2023 kutokana na ushirikiano mzuri baina ya halmashauri na wadau
wa sekta ya elimu.
Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl. Prisca Myalla alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za elimu |
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali
na Msingi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl. Prisca Myalla alipokuwa
akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za elimu katika kikao cha wadau
wa elimu kilichofanyika katika Shule ya Msingi St. Gasper iliyopo jijini
Dodoma.
Mwl. Myalla alisema “Halmashauri ya
Jiji la Dodoma kupitia Divisheni ya Elimu Awali na Msingi imeendelea kufanya
vizuri katika taaluma kupitia matokeo ya mitihani mbalimbali ya kuhitimu elimu
ya msingi na Mtihani wa Upimaji Darasa la Nne. Aidha, shule binafsi zimeendelea
kufanya vizuri kwenye mitihani hiyo na kuchangia ongezeko la wastani wa ufaulu
kutoka wastani 179 kwa mwaka 2022 na kufikia wastani wa 189 kwa mwaka 2023.
Jumla ya watahiniwa 14,907 sawa na asilimia 93.18 waliohitimu elimu ya msingi
2023 walifanikiwa kufaulu na kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2024. Hatua
hii ni ya mafanikio makubwa ukilinganisha na hali ya ufaulu wa mwaka 2022
ambapo asilimia ya ufaulu ilikuwa 89.90”
Kuhusu
elimu jumuishi, alisema kuwa halmashauri inatekeleza Elimu Maalum na Jumunishi
katika shule 61 zinazopokea wanafunzi wenye mahitaji maalum. “Kati ya shule
hizo zenye vitengo ni 11 (Hombolo Bwawani, Mpunguzi, Mlezi, Kisasa, Nala,
Chinangali, Nzunguni B, Generali Msuguli, Mbwanga, Nkuhungu na Ndachi) shule
maalum moja ya Dodoma Viziwi na shule 50 ni Jumuishi” alisema.
Akiongelea utatuzi wa changamoto ya miundombinu ya
madawati na maji katika shule za awali na msingi, alisema kuwa halmashauri
inaendelea kuzitafutia ufumbuzi. Halmashauri imetenga shilingi 358,890,000 kutoka
mapato ya ndani kwa ajili ya kutengeneza madawati 3,418 katika mkakati wake wa
kupunguza changamoto ya upungufu wa madawati kwa wanafunzi wa shule za
msingi. “Halmashauri
imetenga fedha kwa ajili ya gharama za uchimbaji wa visima kwenye maeneo ya shule
ili kuweza kupatikana kwa huduma ya maji kwa wanafunzi. Halmashauri inaendelea
kulipa madeni ya walimu mbalimbali kama vile likizo, malipo ya wastaafu pamoja
na uhamisho kadri fedha zinavyopatikana kutoka serikali kuu au mapato ya ndani”
alisema Mwl. Myalla.
Katika
kuhakikisha shule zote zinatoa huduma ya chakula shuleni, katika msimu huu wa
mvua shule zote zenye maeneo ya kulima zimeagizwa zilime mazao mbalimbali ya
chakula kama Mtama. “Halmashauri imetenga bajeti ya shilingi 100,000,000 kwa
ajili ya kununua mahindi yatakayoandaliwa na kusagwa ili kugawiwa shuleni kwa
ajili ya uji kwa wanafunzi hasa kwa shule zenye matokeo duni ya mitihani
mbalimbali” alisema Mwl. Myalla.
Kikao
cha wadau wa elimu katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kilifanyika kwa lengo
la kuwapa fursa wadau wa elimu kujadili mafanikio na changamoto za sekta ya
elimu na kutoa zawadi kwa shule zilizofanya vizuri, walimu na wanafunzi na
viongozi walioshiriki katika kuhamasisha elimu katika Mkoa wa Dodoma.
MWISHO
Comments
Post a Comment