CCDO Sichona apongeza Azimio Mfuko wa Lishe Dodoma

Na. Dennis Gondwe, DODOMA

MKUU wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Charity Sichona amepongeza azimio la kuanzisha Mfuko wa Lishe wa halmashauri na kusema kuwa utakwenda kutatua changamoto za lishe.

Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Charity Sichona akipongeza Azimio la Mfuko wa Lishe


Pongezi hizo alizitoa alipokuwa akichangia katika kikao cha wadau wa elimu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kilichofanyika katika Shule ya Msingi St. Gasper iliyopo jijini hapa.

Sichona alisema “nikupongeze na kikao chako kwa kuja na azimio la kuanzisha mfuko wa lishe wa halmashauri. Mfuko huo utaenda kutatua matatizo ya lishe na hata ukatili kwa watoto. Mimi kazi yangu kubwa ni kuongea na makundi maalum na huwa tunaongea na watoto wa kike na unakuta wengi wanadanganyika kutokana na kuwa na njaa shuleni. Watoto wa kike wanadanganywa na vijana waendesha bodadoba, wanadanganywa na makondakta wa daladala na mafundi wa gereji”.

Akiongelea ushirikishaji jamii katika kutatua changamoto za sekta ya elimu alisema kuwa ni jambo la muhimu. “Ushauri wa pili ni kushirikisha jamii katika changamoto za shule. Jamii inaposhirikishwa changamoto katika eneo husika ile changamoto inaweza kupungua na kumalizika kabisa kwa sababu inakuwa sehemu ya utatuzi. Huwa tunashirikisha wazazi na jamii katika masuala ya ujenzi. Ila kwenye masuala ya utoro na lishe unakuta jamii haishirikishwi sana kutoa utatuzi. Nashauri kwa walimu wakuu na maafisa elimu kuweza kushirikisha jamii husika na kwenye mikutano kupata nafasi ya kuongea na jamii ili kuwa na uelewa na makubaliano ya pamoja” alishauri Sichona.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma