DC Shekimweri apongeza Jiji la Dodoma kupandisha ufaulu
Na. Aisha Ibrahim, DODOMA
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir
Shekimweri, amewapongeza wadau na waratibu wa elimu kwa kazi nzuri wanayoifanya
ya kuhakikisha ufaulu wa wanafunzi ngazi ya msingi na sekondari unazidi kupanda
kila siku katika Jiji la Dodoma.
Alitoa pongezi hizo katika kikao cha wadau wa
elimu na kuutambulisha mfuko wa lishe shuleni wa mwaka 2025, kilichofanyika ukumbi
wa Vijana uliopo Kata ya Kiwanja cha Ndege, jijini Dodoma.
Akizungumza katika kikao hicho alisema kuwa,
lengo la Rais wa awamu ya sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuanzisha mpango wa
lishe bora shuleni ni kukuza ufaulu wa wanafunzi na kuenzi kauli za Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, isemayo “Elimu tunayohitaji siyo tu ya
kujua kusoma na kuandika bali ni elimu ya kujenga jamii yetu ya kufanya tuwe na
uwezo wa kufanya kazi na kuleta maendeleo kwa wengine”.
Aliongeza kuwa, chini ya utawala wa Rais wa
awamu ya sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan, serikali imejitahidi kuboresha na
kutekeleza kwa vitendo mtaala mpya wa sera ya elimu ambapo matarajio ni kutoka
kwenye elimu ya kukariri na kuvuka kwenda kwenye elimu ya kuelewa na kujua
mambo kwa uhalisia wake. “Tunaona serikali chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu
Hassan, imeboresha mtaala mpya wa sera ya elimu, uliozinduliwa hapa jijini
Dodoma, lengo ni kutoka zama za kusoma kwa kukariri na kwenda kwenye elimu ya
kuelewa” alisema Alhaj Shekimweri.
Katika hatua nyingine, alifafanua kuwa “serikali
imejitahidi kwa kiasi kikubwa kuongeza ajira kwa watumishi na kuboresha
miundombinu kwa shule za msingi na sekondari kama vile madarasa mapya, nyumbani
za walimu, matundu ya vyoo vya wanafunzi na walimu, maabara za kisasa kwa shule
za sekondari. Hivyo, kwa muktadha huo hatutegemei ufaulu unaopungua dalaja la
kwanza” alisema.
Aidha, aliwaasa wazazi na walimu kusimama
katika ubora wao kuhakikisha Jiji la Dodoma linatokomeza ufaulu wa daraja la
nne na sifuri kwasababu serikali
imeboresha miundombinu na maslahi ya wasimamizi wa elimu." Kila mmoja hapa
kwa nafasi yake akisimama kidete, basi
Jiji la Dodoma hakutakuwa na daraja la nne wala sifuri kwasababu serikali
imejitahidi sana kuwaletea miundombinu rafiki na maslahi ya kila mtu"
alisema Alhaj Shekimweri.
Kwa upande wake mwakilishi kutoka Wizara ya Elimu,
Alkan Mwanga, alieleza kuwa lengo la kuboresha mtaala wa elimu nchini Tanzania
ni kuendana na mabadiriko mbalimbali ya nchi na utandawazi kiujumla. “Lengo la
kuboresha mtaala huu ni kuweza kuendana na mahitaji ya jamii, mabadiliko ya
Sayansi na teknolojia na maendeleo ya mabadiriko ya kisiasa” alisema Mwanga.
Sambamba na hayo alifafanua muundo wa mtaala
mpya wa elimu na kusema kuwa muundo huo hujumuisha kuondolewa kwa mtihani wa
darasa la Saba, upimaji wa mtihani wa kitaifa kufanyika Darasa la Sita, mwanafunzi
atatakiwa kumaliza kidato cha Nne kabla ya kuweza kujiajiri au kuajiriwa. Pia
kuwepo kwa mikondo miwili katika ngazi ya sekondari yaani mkondo wa jumla na
mkondo wa amali (ufundi). Wanafunzi wataweza kuchagua mkondo unaowafaa
kulingana na uwezo wao na malengo yao na wahitimu kutoka mkondo wa amali
watapata vyeti viwili: cheti cha ufundi pamoja na cheti cha masomo ya jumla
ambayo ni muhimu kwa ajili yao kujiajiri au kupata ajira serikalini, alifafanua.
Maboresho ya mtaala mpya wa elimu nchini
Tanzania yanatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika mfumo wa elimu, na
yamepangwa kutekelezwa kuanzia mwaka 2025 ambapo lengo kubwa ni kuhakikisha
kuwa wanafunzi wanapata maarifa yanayohitajika katika soko la ajira.
MWISHO
Comments
Post a Comment