Maboresho ya elimu yapelekea kuongezeka kwa ufaulu katika Shule za Awali na Msingi Dodoma
Na. Nancy Kivuyo, KIWANJA CHA NDEGE
Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi Halmashauri
ya Jiji la Dodoma yafafanua mafanikio ya maboresho ya elimu katika shule za
msingi ambayo inafanya ufaulu wa wanafunzi kuongezeka.
Ufafanuzi huo ulitolewa katika Mkutano
wa Wadau wa Elimu na Utambulisho wa Mfuko wa Chakula na Lishe Shuleni ikiwa ni
sehemu ya kujadili suala la lishe bora kuboreshwa kwa asilimia zote ili taaluma
ya wanafunzi ifikie lengo tarajiwa.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa
Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl. Prisca
Myalla alisema “tunaishukuru serikali yetu kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa
kuboresha elimu na kujenga miundombinu mizuri ambayo kwasasa inasaidia utoaji
wa elimu kuwa mzuri. Katika suala la lishe, tunashukuru mfuko wa chakula na
lishe shuleni kwasababu unasaidia wanafunzi kuhudhuria shuleni hali
inayopelekea mahudhurio kuwa juu ukilinganisha na kipindi cha nyuma”.
Akizungumza kuhusu hali ya ufaulu na jumla
ya shule zilizopo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, alisema kuwa kuna jumla
ya shule 194 ikiwa serikali inamiliki shule 107 shule mbili zikiwa za mchepuo
wa kiingereza na shule za binafsi zikiwa 87. Idadi ya wanafunzi ni 112,699,
mahitaji ya walimu ni 2,504 waliopo ni 1,993. Hivyo, Halmashauri ya Jiji la
Dodoma ina upungufu wa walimu 511.
“Kuna shule zetu kama vile Shule ya
Msingi Amani, Shule ya Msingi Kisasa na Shule ya Msingi Mtemi Mazengo zinaongoza
kwa ufaulu wa kiwango cha juu kwa shule za serikali katika jiji letu la Dodoma.
Ukifuatilia kwa makini, utagundua shule hizi zina hiyo programu ya chakula
shuleni. Kwahiyo, wanafunzi wanapata chakula na hiyo inawaongezea utimamu wa
kufuatilia masomo bila kukosa. Kwahiyo, tathmini bado inaendelea kufanyika ili
kubaini changamoto zilizopo na kuzitatua” alisisitiza Mwl. Myalla.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya
ya Dodoma, Sakina Mbugi aliwapongeza wadau wa elimu, wakuu wa shule na walimu
wakuu kwa kufanya kazi nzuri na kuwataka kuendelea kuisadia serikali ili
kuhakikisha jamii inapata elimu bora na nzuri.
“Nawapongeza walimu na watumishi kwa
kazi nzuri, tunaomba muendelee kuisaidia serikali katika kuisaidia jamii kupata
elimu nzuri, kama kuna mapendekezo ya namna ya kuboresha elimu na lishe katika
shule zetu za msingi msisite kuyaleta ili tuweze kuijenga Dodoma iliyo imara
kitaaluma” alisema Mbugi.
Akizungumza kuhusu utoaji wa lishe
shuleni, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Sebastian Pima
alizungumza kwa kukishukuru kikao kuwa “lishe ni mnyororo wa kutengeneza afya. Hivyo,
ni muhimu kuangalia ni aina gani ya vyakula vinapatikana katika mazingira yetu ili
kujua namna ya kuvitumia. Chakula kinamsaidia mtoto kuongeza usikivu, kuwa na afya
njema lakini pia inasaidia mtoto kuondokana na njaa. Kwahiyo, ili elimu yetu
iendelee kuwa bora na kutufikisha viwango vya juu ni lazima suala la afya na
lishe bora lipewe kipaumbele”.
Wadau wa elimu, afya na lishe walijadili
umuhimu wa chakula shuleni huku wakiiipa kipaumbele kaulimbiu isemayo ‘Mlo
bora, Mustakabali mzuri’ na kusisitiza kuwa chakula chenye lishe shuleni kitamsaidia
mtoto kufanya vizuri katika masomo na ufaulu wa wanafunzi utaongezeka kwa
asimilia zote.
MWISHO
Comments
Post a Comment