Dakika 5 kila Mkutano wa Baraza la Madiwani kupata dondoo za Afya Dodoma
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
Mkutano wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la
Dodoma umetenga dakika tano kwa ajili ya kupata elimu ya masuala mbalimbali ya Afya
ili kuwajengea uelewa mpana madiwani.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Mkutano wa Baraza
la Madiwani, Prof. Davis Mwamfupe baada ya kuwasilishwa taarifa ya umuhimu wa
siku ya Afya na Lishe ya Mtaa (SALIKI) katika mkutano wa Maraza la Madiwani uliofanyika
katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Prof. Mwamfupe alisema alipendekeza kuwa kutokana na
maelezo mazuri yaliyotolewa na Mkuu wa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na
Lishe kuhusu maana na umuhimu wa siku ya afya na lishe ya mtaa na lishe kwa
ujumla kuna haja ya kutenga dakika tano katika kila mkutano wa baraza la
madiwani kupata dondoo muhimu za afya.
Awali akielezea maana ya Saliki, Mkuu wa Divisheni ya Afya,
Ustawi wa Jamii na Lishe, Dkt. Sebastian Pima alisema kuwa Saliki ni siku ya
afya na lishe ya mtaa. “Siku hii ni mjumuisho wa huduma zinazofanyika kwenye
jamii nia ikiwa ni kutoa elimu ya masuala yanayohusu afya. Mafunzo ya uandaaji
chakula kwa kutumia vyakula vinavyopatikana katika maeneo ya jamii husika,
utoaji wa chanjo, kuandaa bustani viroba, afya ya uzazi na kukabiliana na ukatili
wa kijinsia” alisema Dkt. Pima.
Katika mkutano huo, Katibu, Joseph Fungo alizitaja
kata zilizofanya vizuri katika eneo la lishe kuwa ni Chamwino iliyoshika nafasi
ya kwanza ikipewa zawadi ya cheti na shilingi 500,000. Kata ya Ipala mshindi wa
pili ilipewa cheti na shilingi 300,000 na Kata ya Chihanga mshindi wa tatu
ilipata cheti na shilingi 200,000.
Akifafanua alisema kuwa mshindi wa kwanza kigezo ni
kufanya Saliki kwa ubora na kufuata mwongozo. “Mshindi wa pili kigezo ni
kufanya Saliki kwa mitaa yote na mshindi wa tatu kuboresha huduma za Saliki”
alisema Fungo.
MWISHO
Comments
Post a Comment