Wananchi waaswa kujitokeza kwa wingi katika Kliniki ya Ardhi
Na. Aisha Ibrahim, VIWANDANI
Afisa
Maendeleo ya Jamii, Dawati la Msaada wa Kisheria Jiji la Dodoma, Frida Ngowi,
amewataka wakazi wa jiji hilo kujitokeza kwa wingi katika Kliniki ya Ardhi
inayoendelea kutolewa katika eneo la ilipokuwa Manispaa ya zamani kwa lengo la
kupata msaada wa kisheria na kuweza kutambua njia muhimu za kutatua migogoro ya
ardhi na kupata haki stahiki.
Dawati hilo liko chini ya Kampeni ya 'Msaada wa Kisheria wa Mama Samia' ijulikanayo kama “Samia Legal Aid Campaign” ambayo inaongozwa na Wizara ya Sheria na Katiba.
Akizungumzia
kuhusu msaada wa kisheria alisema kuwa lengo ni kuwasaidia wananchi wasiokuwa
na uwezo wa kumudu gharama za Mahakama ili kuweza kutatua changamoto mbalimbali
za Ardhi zanazohitaji msaada wa kisheria. “Lengo letu ni kutatua changamoto
mbalimbali za watu wote wasioweza kupeleka madai yao mahakamani. Hivyo, sisi ni
kiungo kati ya Mahakama na wananchi kupatiwa msaada wa sheria” alisema Ngowi.
Aliongeza
kuwa, watu wote wana haki ya kupata msaada wa kisheria kwa amani na utulivu wa
hali ya juu hivyo wananchi wasisite kujitokeza kwa wingi kuelezea changamoto
zao kwasababu katika nchi ya Tanzania hamna mtu yeyote aliye juu ya sheria. “Niwasisitize
wananchi mjitokeze kuelezea shida zenu kwasababu ni haki yenu na nchi hii
hakuna mtu mkubwa juu ya sheria” alisisitiza Ngowi.
Kwa
upande wake, mkazi wa Kata ya Ipagala, Samson Yaledi, alisema kuwa wamekuwa
wanakutana na changamoto ya kuzungushwa huku na huku kupata hatimiliki na
utambulisho wa viwanja vyao kwa muda mrefu bila kufanikiwa jambo
linalowapekelea kukata tamaa kwasababu idara ya Ardhi imekuwa nyuma katika
kutatua changamoto za Ardhi kwa wakati. “Kuhusu suala la Ardhi sisi wananchi
tunafikia hatua ya kukata tamaa kufuatilia kwasababu wanaohusika na huduma hizi
wanatuzungusha sana bila kufanikiwa kwa wakati” alisema Yaledi.
Pia,
aliwaasa wananchi kuzingatia sheria na taratibu za Ardhi kwa kuacha tabia ya
kuanza ujenzi bila ya kuwa na vibali maalum, kuzingatia mipaka na ramani ya
viwanja husika ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima katika jamii. “Niwaase
wananchi wenzangu kuacha tabia ya kuanza ujenzi bila ya kuwa na vibali kutoka
serikalini kwasababu kufanya hivyo ni kusababisha migogoro katika jamii na pia
ni uvunjaji wa sheria na taratibu za nchi” alisema Yaledi.
Nae,
mkazi wa Kata ya Kilimani, Haruna Kifimbo, aliomba serikali kutafuta njia
mbadala ya kuwashirikisha watendaji na wenyeviti wa mitaa kushiriki katika
Kliniki ya Ardhi kwasababu wao ndiyo washughulikiaji wa mwanzo wa kero za Ardhi
kabla ya kufikisha ngazi za juu. “Mimi kama mwananchi naiomba serikali
iwashirikishe hata viongozi wetu wa mitaa na watendaji nao waweze kuwa miongoni
mwa kliniki hii kwasababu ndiyo wanaoshughulikia kesi zetu mwanzo kabisa kabla
ya kufika juu” alisema Kifimbo.
Aidha,
alishauri kuwa ni vema wasimamizi wa kliniki hiyo wangekuwa wanatoka mikoa
mingine, nje ya Jiji la Dodoma, kuja kusikiliza malalamiko yao na kuweza
kuyatatua kwasababu baadhi ya changamoto zao zinasababishwa na wasimamizi
haohao waliowekwa kusimamia kliniki hiyo. “Nitoe ushauri kwa serikali kuleta
wasimamizi wa Kliniki ya Ardhi kutoka mikoa mingine mfano Singida na Morogoro
ili waweze kuendesha hili zoezi kwasababu hawa waliotuwekea hapa ndiyo
wasababishi wakubwa wa migogoro ya Ardhi na changamoto nyingine kama hizo”
alishauri Kifimbo.
Kliniki
ya Ardhi iliyoandaliwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma imelenga kutatua changamoto
mbalimbali za Ardhi kwa kutoa huduma zifuatazo; umiliki wa ardhi, huduma za mipango
miji, upimaji wa Ardhi, huduma za uthamini, vibali vya ujenzi, migogoro ya Ardhi
na huduma za maliasili.
MWISHO
Comments
Post a Comment