DC Shekimweri apongeza Kliniki ya Ardhi jijini Dodoma
Na. Aisha Ibrahim, VIWANDANI
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir
Shekimweri, ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kurejesha tena
Kliniki ya Ardhi inayolenga kutatua kero na changamoto mbalimbali za wananchi
zinazohusiana na masuala ya Ardhi.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri akisisitiza jambo |
Pongezi hizo alizitoa wakati wa ufunguzi wa
zoezi la Kliniki ya Ardhi lililoanza leo na kuendelea mpaka tarehe 28 Februari,
2025, eneo la Halmashauri ya Manispaa ya zamani, jijini Dodoma.
Akizungumzia kuhusu umuhimu wa kliniki hiyo,
Alhaj Shekimweri alisema kuwa ni vema kufanya tathmini ya kero mbalimbali za Ardhi
zilizopita na kuzitafutia ufumbuzi kabla ya kusikiliza kero mpya kwasababu
itakuwa ni sawa na kufanya kazi bure kuzungumzia kero moja kila wakati. “Ni vema
kufanya tathmini ya mazoezi yaliyopita kwasababu pengine kuna mtu zoezi
lililopita alikuwepo na hili yupo kwa changamoto ile ile, huenda hajaridhika na
huduma au majibu aliyoyapata kliniki iliyopita ndiyo maana yupo tena” alisema Alhaj
Shekimweri.
"Wataendelea kuja kama
wanaowashughulikia ni miongoni kwa visababishi vya matatizo yao, yaani mtu
anayo kero ya miliki pandikizi alafu anayeishughulikia ndiye aliyesababisha
kupatikana kwa kero hiyo kwahiyo tegemea kumuona kila kliniki kwa changamoto
ile ile lakini pia mnakubaliana kwenda 'site' na baadae inasitishwa kwahiyo
jambo lake ni kama litaanza tena upya, hivyo hapa atakuja mara kwa mara”
aliongeza.
Sambamba na hilo alisema, ni lazima kuwepo na
dawati maalum la kupokea na kusimamia maoni ya wananchi kwa lengo la kukusanya
kero na mapendekezo mbalimbali kutoka kwa wananchi kwasababu jambo hilo
litaepusha kupunguza msongamano wa kero zinazojirudia kila wakati. “Kuwepo na
dawati la kusikiliza na kupokea maoni yetu na ushauri kwasababu tangu nimefika
hapa nimepokea maoni mengi na ni mazuri” alisema Alhaj Shekimweri.
Aidha, alikemea kitendo cha wasimamizi wa Ardhi
kushindwa kutimiza majukumu yao kwa wakati kwa kusingizia changamoto ya mtandao
na aliwataka kuhakikisha tatizo hilo linatatuliwa haraka iwezekanavyo. “Kuna
watu hapa wanataka kusoma, kuangalia hiyo migogoro na hatimiliki mitandaoni,
nunueni mtandao wa kisasa wa bila nyaya 'Wi-Fi' na muweke bango kubwa sehemu
hii lililoandikwa msimbo ili kila mwenye shida ya mtandao aweze kutatua shida
hiyoo na kuepuka visingizio” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, aliomba wazee,
wajawazito na watu wenye ulemavu kupewa kipaumbele na kutengewa eneo maalum katika kliniki
hiyo. “Wazee, wajawazito na watu wenye ulemavu wapewe kipaumbele katika huduma
hii pia watengewe meza maalum, kwahiyo wazee hawa wasiendelee kuomba hisani
kwaajili ya kuhudumiwa kwasababu hatupo hapa kufanya biashara” alisema.
Lakini, aliwasisitiza wananchi kuwa na
nyaraka zenye uthibitisho wa eneo analolishughulikia kwasababu maneno bila uthibitisho
ni mojawapo ya sababu ya kujirudia kwa kero mbalimbali za Ardhi katika kila
kliniki. “Hatuwezi kushughulikia mgogoro ambao mtu anaongea tu bila nyaraka au
uthibitisho halisi, mara oooh! Niliuziwa na mauziano hayapo, mara nilitapeliwa
kiwanja changu na hakuna nyaraka yoyote” alisisitiza Shekimweri.
Alimaliza kwa kushauri kuwa, wananchi
wapatiwe elimu ya kutosha kuhusu haki zao na hatimiliki kwa kufuata misingi ya
kisheria ili kuondoa migogoro ya Ardhi na kama hatoridhika na maamuzi ya
mahakama anayo haki ya kukata rufaa ilimradi haki msingi ipatikane.
MWISHO
Comments
Post a Comment