Diwani Makole asema neno kwa Machinga Dodoma
Na. Shahanazi Subeti, MAKOLE
Diwani wa kata ya Makole, Halmashauri
ya Jiji la Dodoma Omary Haji amewapongeza wafanyabiashara wadogo wadogo (Machinga)
wa Mkoa wa Dodoma kwa kuwa na umoja na mshikamano katika utendaji wa kazi kwa
lengo la kujikwamua kiuchumi.
Aliyasema hayo wakati wa makabidhiano rasmi ya Ofisi ya Viongozi wa Machinga Mkoa wa Dodoma iliyojengwa Kata ya Makole ambayo imegharimu shilingi milioni 56 zikiwa ni jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa Machinga katika taifa.
Haji alisema “nawashukuru sana Machinga
wa Mkoa wa Dodoma, wakiongozwa na wenyeviti wao na viongozi wengine kwa kuweza
kuungana katika kufanikisha ujenzi wa ofisi hii na kwakuwa Dkt. Samia Suluhu
Hassan ameweza kuwatambua Machinga wa Dodoma na kuwajengea ofisi katika eneo
hili linaweza kuwasaidia na kuwarahisishia shughuli zenu za kibiashara. Kwahiyo,
ni wazi kabisa mtalitunza na kulithamini vizuri jengo hili”.
Sambamba na hilo alimpongeza Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa utu na kuthamini
wafanyabiashara wadogo wadogo (Machinga) kwa kufanya mapinduzi katika Kata ya
Makole. “Kwahiyo, nina imani kabisa mtalienzi vizuri jengo hili na kama
mnavyoliona jengo ni la kisasa zaidi na mmewekewa 'furniture' nzuri lakini
mmependezeshewa na jengo lenu ni zuri kuliko hata ofisi ya kata” alisema Haji.
Pia aliongezea kwa kuwataka Machinga kuweza
kuwa makini na miundombinu ya ofisi ili iendelee kuwa imara zaidi. “Leo
tunaikabidhi ofisi hii, ambayo ndani imekamilika kila kitu, sasa ni jukumu lenu
kuweza kusimamia vizuri kwa umakini na kuweza kuhakikisha kwamba vitu
vyote vilivyopo hapa vipo salama. Lakini
kutunza mazingira ya eneo lenu la kazi kwa kupanda miti, nina imani kabisa kwa
umoja wenu hili jengo linaenda kuwa jipya siku zote. Pia muweze kushirikiana na
wenzenu ambao wapo hapa, kuwepo kwenu kwenye Kata ya Makole kunaweza kuchangia
haswa maendeleo katika soko letu” alisema Haji.
Mkuu
wa Divsheni ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Charity
Sichona, alielezea kuwa ujenzi wa Ofisi ya Machinga Mkoa wa Dodoma Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa agizo kwa
serikali kwamba kila mkoa kujenga ofisi kwa ajili ya viongozi wa Machinga kwa lengo
la kurahisisha utoaji huduma kwa wafanyabiashara hao. “Kwahiyo, mara ya kwanza
alitoa shilingi milioni 10 kwa kila mkoa kwa kuanza ujenzi. Baada ya ile shilingi
milioni 10 kukamilisha ujenzi wake, Halmashauri ya Jiji la Dodoma iliongezea shilingi
milioni 26.2 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi. Hadi kufikia hatua ya kukamilika kwa
jengo hili jumla ya shilingi milioni 56 zimetumika” alisema Sichona.
Pia alimalizia kwa kusema kuna haja ya wafanyabiashara wadogo wadogo kuweza kupata huduma kutoka kwa viongozi wao. “Sasa tuwakibidhi viongozi waweze kutumia ofisi hii kutoa huduma kwa wafanyabiashara wao. Pia shughuli za uzinduzi rasmi zitakuja kufanyiwa na viongozi wakubwa. Lakini sasa hivi tukabidhi kwasababu kumekuwa kuna uhitaji wa wafanyabiashara wadogo wadogo kupata huduma kwa haraka zaidi” alisema Sichona.
Nae Mwenyekiti wa Christian Msumari,
alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan
kwa kufanya jambo kubwa lenye kuleta tija katika maendeleo ya Machinga ya kuwa
na ofisi ya kusemea kero zao. “Kwasababu hapo mwanzo tulikuwa hatuna sehemu
yoyote ya kutolea huduma zetu, lakini kwasasa hivi limekuja jambo la kheri na
ni jambo zuri la serikali ya awamu ya sita kwa kututambua na kutuheshimisha, kutujengea
ofisi zetu na sehemu za kutolea huduma kama viongozi. Mwanzoni tulionekana kama
wahuni, ila sasahivi tunaonekana ni wafanyabiashara wadogo wadogo ambao tupo
kwenye mpango wa kukua kwenda kuwa wafanyabiashara wakubwa” alisema Msumari.
Aidha, Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa
matunda katika Soko la Makole, Denis Athumani, aliishukuru serikali kwa kuona
mchango wa wafanyabiashara wadogo wadogo katika kuleta maendeleo. “Vilevile,
tunamshukuru kwa kutuletea katika eneo letu la kata ya Makole ambapo nasisi
tunaungana na wenzetu katika harakati zetu za utafutaji. Kwahiyo, tunashukuru
serikali kwa kutambua umuhimu wetu na fursa hii waliyotupa ili mradi mawazo
yetu ya pamoja tuungane katika eneo moja kwa lengo la kuyafikisha ndani ya
serikali” alisema Athumani.
MWISHO
Comments
Post a Comment