Dodoma Jiji FC, mbioni kuwakabili Nyuki wa Tabora


Na. Mussa Richard, TABORA

Klabu ya Soka ya Dodoma Jiji FC, imewasili salama mkoani Tabora, ambapo mchana wa kesho watakuwa na kibarua cha kuikabili klabu ya soka Tabora United, (Nyuki wa Tabora) katika mchezo wa Ligi kuu ya NBC Tanzania bara, mchezo utakao vurumishwa majira ya saa 8 kamili mchana katika dimba la Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora.



Akizungumza katika mkutano na waandishi wa Habari Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji FC, Meck Mexime alisema “Mungu ametusaidia tumefika salama, maandalizi yote ya mchezo tulifanya tukiwa Dodoma, hapa tunakuja katika utekelezaji tu wa kile tulichokifanyia mazoezi, tunajua tunakuja kukutana na mpinzani mgumu. Lakini na sisi tumejiandaa katika mazingira yote kukabiliana nao, ukizingatia tunaelekea mwishoni mwa msimu. Kwahiyo, sisi kama Dodoma Jiji FC, tumejiandaa tuwe bora zaidi ili tuweze kupata matokeo mazuri na tuweze kuondoka na alama zote tatu”.

Nae, Augustine Nsata, ambaye ni Nahodha wa Klabu ya Soka ya Dodoma Jiji FC, akaweka wazi utayari wa kikosi kuelekea katika mchezo wa kesho dhidi ya Tabora United.



“Kama wachezaji tumejiandaa vizuri kuelekea katika mchezo wa kesho na tunajua utakuwa ni mchezo mgumu kwa pande zote mbili, lakini sisi tumejiandaa kwenda kufanya vizuri ili tuweze kujiweka katika sehemu nzuri zaidi kwenye msimamo wa ligi. Pia niwaombe mashabiki wa Dodoma Jiji FC, popote pale walipo waendelee kutuunga mkono kwasababu wao ni nguzo muhimu sana kwetu ya kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye kila mchezo tunaocheza” alisema Nsata.

Dodoma Jiji FC, kwasasa ipo katika nafasi ya Saba katika msimamo wa ligi kuu ya NBC Tanzania bara ikikusanya alama 26, ikicheza michezo 20 huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi.

MWISHO

 

Comments

Popular Posts

Mbunge Mavunde akabidhi Kompyuta kwa Kata 41 za Jiji la Dodoma

Wafanyabiashara wa Soko Kuu la Majengo Dodoma watarajia makubwa Mradi wa TACTIC

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma