Matenga yageuka lulu kilimo cha mbogamboga Dodoma
Na. Mwandishi wetu, NZUGUNI Wananchi wanaoishi mijini, hususan kwenye nyumba za kupanga wametakiwa kutumia matenga, makopo ya maji na matairi yaliyotumika kuanzisha bustani za mbogamboga majumbani ili kujihakikishia upatikanaji wa chakula salama, kupunguza gharama za maisha na kuhifadhi mazingira. Wito huo ulitolewa na Afisa Kilimo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Zaidina Juma wakati wa maonesho ya 32 ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Malecela mjini Dodoma. Alisema kuwa kilimo cha kwenye matenga ni njia rahisi inayosaidia kuhifadhi mazingira huku kikitatua changamoto ya upatikanaji wa maeneo ya kulima. Alisema kuwa wananchi wengi wanaishi kwenye nyumba za kupanga au maghorofani ambako hakuna nafasi ya kuanzisha bustani za kawaida, lakini bado wanaweza kuzalisha mboga zao kwa kutumia vifaa vinavyotupwa na kula mboga zenye usalama, tofauti na baadhi ya mazao yanayouzwa sokoni ambayo wakati mwingine huvunwa muda mfupi baada ya kunyunyiziwa viuatilifu. ...