MEMKWA daraja kwa watoto waliokosa elimu rasmi
Na. Mwandishi wetu, DODOMA
Wananchi wa Jiji la Dodoma wametakiwa kuhakikisha
watoto waliokosa kuanza elimu rasmi kwa wakati hawabaki nyuma, bali watumie
fursa ya Elimu ya Watu Wazima na Mfumo wa Elimu Nje ya Mfumo Rasmi (MEMKWA)
kupata elimu na kujenga msingi bora wa maisha yao.
Wito huo ulitolewa na Mwenyekiti wa Maafisa Elimu Jiji la Dodoma, Yassin Mponda katika Maadhimisho ya Wiki ya Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi (MEMKWA) yanayofanyika katika Viwanja vya Mapumziko vya Nyerere Square, ambapo shughuli mbalimbali zinaendelea kuanzia tarehe 17 hadi 21 Agosti, 2026.
Mponda alisema kuwa elimu ya watu wazima ina nafasi
kubwa katika kuwapatia wananchi waliokosa fursa ya elimu rasmi uwezo wa kusoma,
kuandika, kuhesabu pamoja na kupata ujuzi unaowawezesha kujitegemea na
kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.
Aliongeza kuwa mtoto anayepaswa kuanza Darasa la
Kwanza akiwa na umri wa miaka sita, lakini akakosa fursa hiyo na baadaye
kufikisha umri mkubwa zaidi, anaweza kujiunga na elimu nje ya mfumo rasmi
badala ya kuachwa nje ya mfumo wa elimu.
“Ni wakati wetu sasa kuhakikisha tunawaleta waliokosa
elimu rasmi na wamevuka ule umri wa kuanza masomo waje mashuleni wapate elimu,”
alisema Mponda.
Aidha, alitoa wito kwa wazazi, viongozi na jamii kwa
ujumla kushirikiana katika kuwatambua na kuwahamasisha watoto hao kutumia fursa
za elimu zinazopatikana, akisisitiza kuwa MEMKWA ni daraja muhimu la kuwasaidia
waliochelewa kuanza shule kupata elimu na kujenga msingi wa maisha bora ya
baadae.
Maadhimisho hayo yanalenga kuibua mafanikio, changamoto
na fursa zilizopo katika utoaji wa elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo
rasmi, huku jamii ikihimizwa kuchangamkia fursa hizo kwa kuwa maarifa na ujuzi
ni msingi muhimu wa maendeleo endelevu ya mtu binafsi, familia na taifa.
MWISHO
Comments
Post a Comment