Timu ya Watumishi Jiji la Dodoma yadaiwa ushindi mashindano ya SHIMISEMITA

Na. Lulu Luvanda, DODOMA

Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeiaga timu ya watumishi itakayoliwakilisha jiji hilo katika Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Serikali za Mitaa (SHIMISEMITA) 2026 yatakayofanyika jijini Mbeya na kutakiwa kurejea na ushindi.



Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko alipokuwa akiiaga timu hiyo katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri.

Akizungumza katika hafla ya kuwaaga wachezaji hao jijini Dodoma, alisema kuwa mashindano hayo ni fursa ya kulitangaza Jiji la Dodoma kupitia michezo, huku akiwataka wachezaji hao kuzingatia nidhamu, maadili na misingi ya utumishi wa umma.

Aliwakumbusha umuhimu wa michezo katika kuimarisha afya, mshikamano na uhusiano miongoni mwa watumishi, huku akiwataka kulitangaza vizuri Jiji la Dodoma kwa kuonesha uwezo, nidhamu na ushindani wa hali ya juu.



Kwa upande wake Meneja wa Timu ya watumishi wa Jiji la Dodoma, Dkt. Sebastian Pima alisema kuwa wamefurahia kumuona Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma akikutana na timu nzima na kuwapa maneno ya hamasa kabla ya kuelekea kwenye mashindano ya SHIMISEMITA. Aliishukuru ofisi ya mkurugenzi kwa uungaji mkono unaotolewa kwa timu hiyo, hatua inayochochea maandalizi na hamasa kubwa ya kushiriki kwa lengo la kupata ushindi.

Alisema kuwa wanatambua Dodoma ni Fahari ya Watanzania, hivyo timu pamoja na safu ya uongozi ipo tayari kuhakikisha inaiwakilisha na kuifaharisha Dodoma katika mashindano hayo. Alisisitiza kuwa umoja, maandalizi na dhamira ya ushindi ni muhimu katika kufanikisha lengo hilo.




Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, mchezaji mwandamizi Leonard Mkinga alisema kuwa timu imejiandaa vizuri ikiwa na dhamira ya kurejea Dodoma na matokeo mazuri. Alisema kuwa nia, maandalizi na nidhamu kuwa nguzo muhimu za mafanikio.

Timu hiyo yenye jumla ya wachezaji 60 inatarajiwa kushiriki mashindano hayo kwa siku 15, kuanzia tarehe 16 Agosti, hadi tarehe 28 Agosti, 2026.

Comments

Popular Posts

Timu ya Watumishi Jiji la Dodoma inayoshiriki SHIMISEMITA yatakiwa kurejea na ushindi

Dodoma Jiji yajiandaa Ngoma na Kwaya SHIMISEMITA, 2026

Barabara za Mtaa wa Mbwanga yafunguliwa, Diwani Kerenge aitaja kuwa chachu ya maendeleo