Timu ya Jiji la Dodoma yatakiwa kuzingatia uzalendo michezo ya SHIMISEMITA

Na. Mwandishi wetu, DODOMA

 

Jumla ya wanamichezo 60 wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, wakiwemo makocha wanne, wametakiwa kuzingatia nidhamu na uzalendo katika Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Serikali za Mitaa Tanzania (SHIMISEMITA) yanayofanyika mkoani Mbeya ili kulinda hadhi ya makao makuu.

 


Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko katika hafla fupi ya kuwaaga wanamichezo hao iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri.

 

Aliwataka kuitumia michezo hiyo kuiwakilisha Dodoma kwa nidhamu, uzalendo na kujiamini, wakitambua kuwa wanatokea makao makuu ya nchi. “Nendeni mkifahamu kuwa mnatokea makao makuu ya nchi. Nendeni mkalete tabasamu kwa Watanzania na si huzuni, maana Dodoma ni fahari ya Watanzania. Nidhamu ni miongoni mwa sababu zilizochangia mafanikio ya mwaka jana. Hivyo, dumisheni nidhamu, kufuata misingi ya utumishi wa umma na kulinda hadhi ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma,” alisema Dkt. Sagamiko.

 

Aidha, alimpongeza Afisa Michezo wa Jiji la Dodoma, Neema Kilongola kwa juhudi na kazi kubwa anayoifanya katika kuandaa na kuendeleza michezo mbalimbali, huku akimtaka kuongeza ubunifu zaidi. Alisema kuwa jiji lina imani kubwa na timu hiyo na linatarajia ushindi wa jumla pamoja na vikombe mbalimbali kati ya halmashauri 184 zinazoshiriki mashindano hayo.

 


Awali, akisoma taarifa fupi ya maandalizi ya kuelekea michezo ya SHIMISEMITA, Afisa Michezo wa Jiji la Dodoma, Neema Kilongola alisema kuwa timu hiyo yenye wanamichezo 60 na makocha wanne itashiriki michezo 15, ikiwemo netiboli, mpira wa miguu, mpira wa wavu, mpira wa kikapu, ngoma, kwaya, pool table, drafti, darts, kizazi kipya, bao, uchoraji na kuvuta kamba.

 

Alisema kuwa timu hiyo imejiandaa vema kwa ajili ya mashindano hayo na ina dhamira ya kuiwakilisha Halmashauri ya Jiji la Dodoma, huku wanamichezo wakitakiwa kutumia mashindano hayo kuonesha vipaji, nidhamu na uwezo wao katika kulinda hadhi ya Dodoma kama makao makuu ya nchi.

Comments

Popular Posts

Dodoma Jiji yajiandaa Ngoma na Kwaya SHIMISEMITA, 2026

Barabara za Mtaa wa Mbwanga yafunguliwa, Diwani Kerenge aitaja kuwa chachu ya maendeleo

Timu ya Watumishi Jiji la Dodoma inayoshiriki SHIMISEMITA yatakiwa kurejea na ushindi