Jiji la Dodoma lashauriwa kulinda hadhi ya Makao Makuu ya Nchi

Na. Mwandishi wetu, DAR ES SALAAM

 

HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeshauriwa kuendelea kusimamia Mpango Kabambe wake ili kuhakikisha jiji linakuwa na mpangilio wa kisasa na kulinda hadhi ya makao makuu ya nchi.

 

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Jenifa Omolo (kushoto) akiongea na wataalam wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Jenifa Omolo alipotembelea banda la Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwl. Julius Nyerere jijini hapa.

 

Alisema kuwa ukuaji wa Jiji la Dodoma unapaswa kwenda sambamba na upangaji bora wa maeneo, miundombinu na mazingira ya mji ili kuongeza mvuto zaidi kwa wakazi, wawekezaji na wageni wanaofika kwa shughuli mbalimbali za kiserikali na kiuchumi.

 

Alisisitiza kuwa taswira ya mji ambao ni makao makuu ya nchi inapaswa kuonekana wazi kupitia mpangilio wa kisasa, unaozingatia uzuri wa mji, matumizi sahihi ya ardhi na maendeleo yanayopangika na yanapaswa kuendana na kutenga maeneo ya shughuli za kiuchumi za vijana ambao ndio taifa la kesho.

 

Hivyo, utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni jambo muhimu sana kwa mustakabali wa sasa na wa kesho.

 


Kwa upande wake, mwananchi aliyetembelea banda la Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika Maonesho ya Sabasaba, Omary Nyange alisema kuwa amefurahia kupata majibu ya maswali yake kuhusiana na fursa za viwanja katika jiji hilo. Aidha, aliipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kushiriki katika maonesho hayo.

Halmashauri ya Jiji la Dodoma inashiriki katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, kuanzia tarehe 28 Juni hadi 13 Julai 2026 chini ya kaulimbiu isemayo “Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba ni Fahari ya Tanzania”.

 

Comments

Popular Posts

Afisa Biashara Arusha apongeza ukuwaji wa Biashara wa Jiji la Dodoma

Jiji la Dodoma latangaza fursa za Uwekezaji katika Maonesho ya Sabasaba, 2026