Kata ya Mnadani watakiwa kuandikisha watoto Darasa la Kwanza
Na. Dennis Gondwe, MNADANI
JAMII imetakiwa kuhakikisha
watoto wenye umri wa kuandikishwa shule za msingi wanaandikishwa kwa wakati
waweze kupata elimu kwa mujibu wa sheria.
![]() |
Wanafunzi wakiwa darasani (picha kutoka maktaba) |
Kauli hiyo ilitolewa na
Afisa Elimu Kata ya Mnadani, Robert Tesha alipokuwa akiongea kwenye mkutano wa
hadhara wa wananchi wa Mtaa wa Mnadani katika Kata ya Mnadani jijini Dodoma.
Tesha alisema “zoezi la
uandikishaji kwa shule za msingi limeanza tangu mwezi Oktoba mwaka huu. Watoto
wanaoandikishwa ni darasa la awali kuanzia miaka minne hadi mitano na darasa la
kwanza miaka sita hadi nane na uandikishaji hauna gharama yoyote. Mzazi unapokwenda
unatakiwa kwenda na cheti cha mtoto cha kuzaliwa na kama hauna unapitia kwa Afisa
Mtendaji wa Mtaa anakuandikia barua na majina kamili ya mwanafunzi kwa sababu
majina yanaingizwa kwenye mfumo na hilo jina halitabadilika mpaka chuo kikuu.
Niombe sana waleteni watoto tuwaandikishe shule, madarasa yameshajengwa na mama
Dkt. Samia Suluhu Hassan sasa hivi tunahitaji watoto tuwaandikishwe na mwisho
wa kuandikisha ni tarehe 31 Desemba, 2023 tunapofungua shule tarehe 8 Januari,
2024 ni kusoma tu” alisisitiza Tesha.
Wakati huohuo, alikemea
uanzishaji wa shule kiholela katika mitaa ya Kata ya Mnadani. “Niombe huku
mtaani katika Kata ya Mnadani kuna vishule vidogo vidogo. Hivyo, haviruhusiwi,
lazima uwe na kibali na kusajiliwa, kuna wengine wakiniona wanakimbia, shule za
awali kata nzima ya Mnadani zilizosajiliwa ni tano tu, wengine wote hawajasajiliwa.
“Naomba tuwaandikishe watoto kwenye shule rasmi. Shule zetu zote za serikali za
msingi zina madarasa ya awali, tuwapeleke watoto huko, kwenye shule hizo zenye
usajili rasmi, watoto wanapokwenda darasa la kwanza wanajua kusoma na
kuandika.” alisema Tesha.
MWISHO
Comments
Post a Comment