Bodaboda ni kazi, epukeni uhalifu
Na. Dennis Gondwe, MNADANI
VIJANA waendesha Pikipiki
(bodaboda) katika Kata ya Mnadani wametakiwa kuichukulia kazi ya kuendesha
pikipiki kama kazi nyingine na kujiepusha na kujiunga kwenye makundi ya
uhalifu.
![]() |
Picha kutoka mtandaoni |
Kauli hiyo ilitolewa na Mkaguzi
Msaidizi wa Polisi, Focus Ishika alipokuwa akiongea na wananchi wa Mtaa wa
Mnadani katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika mtaa huo.
Mkaguzi Msaidizi Ishika
ambae pia ni Polisi Kata ya Mnadani alisema kuwa vijana waendesha bodaboda
wanakosa elimu ya umuhimu wa kazi wanayofanya. “Vijana wetu wa bodaboda
wanakosa elimu juu ya umuhimu wa kuichukulia kazi ya bodaboda kama kazi
nyingine. Wazazi wenye watoto wanaoendesha pikipiki toeni elimu kwa vijana wenu
ajira ya udereva pikipiki waichukulie kama yule anayeamka asubuhi na kwenda
benki au kwenda kufundisha (mwalimu) wanatakiwa kuifanya kazi hiyo kwa moyo na
bidii. Kwa hiyo makosa tunayo sisi. Mwanao anatoka asubuhi na pikipiki hujui
anapaki kituo gani, hujui rafiki zake nani, hujui mishemishe zake ni zipi,
unakuja kupewa taarifa kuwa mwanao yupo Polisi amekamatwa unakuja juu, mwanangu
siyo mwizi unamjua mwanao vizuri kweli??” alihoji Mkaguzi Msaidizi Ishika.
Aidha, aliwashauri wananchi
kuwa wanapopewa taarifa za uhalifu dhidi ya watoto wao kuzifanyia kazi. “Mimi
niwaombe, tujaribu kupendana unapopewa taarifa juu ya mwanao ifanyie kazi
kuliko kukurupuka kukasirika. Hakuna anayemjua mwanao kama walimwengu, na
walimwengu ndiyo sisi” aliongeza.
Alishauri mabalozi kuwa na
taarifa sahihi za vijiwe vya bodaboda na usajili wake. “Tusaidiane kuvuka huu
mwaka salama sisi pamoja na watoto wetu, usimuonee muhari. Kila balozi
anawajibu kupita kwenye kila kituo cha bodaboda kuhakikisha anakikagua,
anawajua vizuri waendesha bodaboda na vituo vimesajiliwa. Utaratibu sio mgumu
wa kusajili kituo cha bodaboda, unachukua barua kwa Afisa Mtendaji unaenda
Latra kituo kinapewa jina na kusajiliwa na idadi inajulikana ni watu 15”
alisisitiza.
Vilevile, alishauri kaya
kuwa na filimbi kwa ajili ya usalama wao. “Mzee mwenzangu huna filimbi? kuwa na
filimbi ili linapotokea piga filimbi watu watoke watoe msaada. Nikisema wangapi
wanafilimbi nyumbani kwao hapa nitapata wachache. Kuwa na filimbi na tochi
nyumbani kwako kwa ajili ya ulinzi wako binafsi. Mfano, ukiwa na tochi,
umesikia kishindo nje, mulika atakimbia tu hakuna mwizi anaependa mwanga,
lazima atakimbia tu” alishauri.
MWISHO
Comments
Post a Comment