Afisa Mifugo Kata ya Mnadani anaupiga mwingi
Na. Dennis Gondwe, MNADANI
KATA ya Mnadani inajivunia
utendaji kazi wa Afisa Mifugo kwa kuhakikisha wananchi wanakuwa na mifugo yenye
afya kutokana na kupata huduma zote za chanjo kwa wakati.
![]() |
Afisa Mifugo Kata ya Mnadani, Elizabeth Shirima |
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa
Mtendaji Kata ya Mnadani, Caroline Massawe alipokuwa akitoa taarifa ya
mafanikio ya Kata ya Mnadani kwa kipindi cha miaka mitatu (2021-2023) katika
mkutano wa hadhara wa wananchi wa Mtaa wa Mnadani.
Massawe alisema “nikiwa
Afisa Mtendaji wa Kata ya Mnadani, napenda kumpongeza Afisa Mifugo wa Kaya ya
Mnadani, anajitahidi kwa kweli kutekeleza majukumu yake ya kazi anajituma na ni
muwajibikaji mzuri sana. Kwa wale wanaofuga natumaini wanalitambua hilo,
anawatembelea wananchi kuchanja mifugo yao kwa wakati na mbwa wanaozurura
anawachanja pamoja na majukumu mengine, mama huyu anaupiga mwingi”.
Akiongelea mafanikio ya
sekta ya mifugo, alisema kuwa sekta hiyo imefanikiwa kudhibiti magonjwa ya mlipuko
na magonjwa mengine yanayosababishwa na kupe kwa kutoa elimu kwa wafugaji. “Chanjo
mbalimbali za mifugo kama homa ya mapafu kwa ng’ombe, kichaa cha mbwa, kuku pia
kuhamasisha wafugaji kuunda vikundi vya wafugaji ng’ombe na kuku. Jumla ya
vikundi 11 viliundwa na kupata mikopo kutoka Halmashauri ya Jiji. Vikundi vya
ufugaji ng’ombe wa maziwa vitano, vikundi vya ufugaji kuku wa mayai viwili na vikundi
vya ufugaji kuku wa nyama vinne” alisema Massawe.
Alisema kuwa kata
imefanikiwa kuendesha zoezi la utambuzi wa mifugo na kutoa elimu na kuhamasisha
ufugaji bora. “Jumla ya ng’ombe 304 na mbuzi 132 waliweza kutambuliwa na
kuvishwa hereni za utambuzi. Elimu ya ufugaji bora wa mifugo hasa ndani ya mabanda,
uogeshaji mifugo, uhifadhi wa malisho, matumizi ya vyakula vya ziada na ufugaji
wanyama wadogo kama sungura ilitolewa kwa wafugaji” alisema Massawe.
MWISHO
Comments
Post a Comment