Mnadani yaweka kipaumbele ulinzi na usalama
Na. Dennis Gondwe, MNADANI
WAKAZI wa Mtaa wa Mnadani
katika Kata ya Mnadani wametakiwa kuweka kipaumbele swala la ulinzi na usalama
ili jamii iwe salama katika kipindi cha sherehe za mwisho wa mwaka.
![]() |
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mnadani, Hema Wawa akisisitiza jambo |
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti
wa Mtaa wa Mnadani, Hema Wawa alipokuwa akiwahutubia mamia ya wananchi wa Mtaa
wa Mnadani katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika mtaa huo.
Wawa alisema “tunapoelekea
katika sherehe za Krismasi na mwaka mpya, niwaombe sana wananchi wangu msiache makazi
bila mtu anayebaki nyumbani. Kipindi hicho kina mkesha, unakuta watu wamefunga
nyumba wameenda kwenye mkesha, unarudi nyumbani unakutana na kitu ambacho
hukutegemea. Tuchukue tahadhari, kama mnaenda kwenye mkesha mjipe ratiba,
wengine waende kwenye mkesha na wengine wabaki waende ibada ya asubuhi. Ulinzi
unaanzia kwako mwenyewe kujilinda wewe na mali yako. Niwaombe sana tulisimamie
hili ili kuepuka changamoto zinazoweza kudhibitiwa”.
Aidha, aliwatakia heri ya Krismas
na Mwaka mpya, 2024 wananchi wa Mtaa wa Mnadani. “Mwisho niwashukuru wananchi
wangu kwa uvumilivu wenu, kwa kuacha shughuli zenu na kujitokeza kwa wingi
kwenye mkutano huu wa hadhara. Niwaombe sana mabalozi, muendelee kuwapa taarifa
wananchi wetu, kuna baadhi wanasema hatujaalikwa, wapeni taarifa. Mkutano kama
huu wa hadhara tunapokea maoni yenu na ushauri ili twende pamoja, maendeleo
hayawezi kuletwa na mtu mmoja. Tukishirikiana kwa pamoja tunajenga mtaa wetu,
kata yetu, wilaya yetu na mkoa wetu, lakini tunajenga taifa letu la Tanzania.
Na kufanya hivyo, tutakuwa tumemsaidia Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu
Hassan katika kutekeleza miradi mbalimbali. Mwisho nichukue nafasi hii
kuwatakia heri ya Krismas na Mwaka mpya 2024” alisema Wawa.
MWISHO
Comments
Post a Comment