Serikali awamu ya sita yaipaisha Mnadani
Na. Dennis Gondwe, MNADANI
SERIKALI ya awamu ya sita
inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha nyingi za
kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta ya elimu kwenye Kata ya Mnadani ikiwa
ni pamoja na ujenzi wa shule mpya za msingi zinazojengwa kwenye Kata ya Mnadani
hii imesaidia kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia.
![]() |
Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania |
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa
Mtendaji Kata ya Mnadani, Caroline Massawe alipokuwa akielezea mafanikio ya
serikali ya awamu ya sita katika mkutano wa hadhara wa wananchi wa Mtaa wa Mnadani
uliofanyika katika ofisi ya kata hiyo.
Massawe alisema kuwa kwa
asilimia kubwa mafanikio mengi ya sekta ya elimu katika Kata ya Mnadani yametokana
na serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu
Hassan. Mafanikio katika sekta ya elimu ni uongezekaji wa miundombinu shuleni,
idadi ya wanafunzi imeongezeka, shule mpya kuanzishwa, mafunzo ya walimu kazini,
aliongeza. “kupitia serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt.
Samia Suluhu Hassan, Kata ya Mnadani kupitia Shule ya Msingi Mbwanga tumepokea
fedha shilingi 318,800,000 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya msingi Jitegemee
yenye vyumba tisa vya madarasa, jengo la utawala na matundu 18 ya vyoo, ujenzi
umekamilika na sasa wanafunzi wanaendelea na masomo na hii imetokana na
ongezeko kubwa la wanafunzi Shule ya Msingi Mbwanga kutokana na ongezeko hilo
serikali ya awamu ya sita imeona ni vema ikapatikana shule mpya ili iweze
kusaidia wanafunzi. Ujenzi huu wa shule mpya umesaidia kuodoa msongamano Shule
ya Msingi Mbwanga, imesaidia kupunguza kutembea kwa umbali mrefu kwa watoto
kwenda Shule ya Msingi Mbwanga, shule mpya imesaidia watoto wa kata jirani kuja
kusoma pale kama Chang’ombe na Miyuji na shule hii ya mpya ya Jitegemee
imechukua watoto kutoka mtaa jirani wa Ndachi, Mnadani, Miyuji na Chang’ombe B.
Kwa ambao hamjafika Shule mpya ya Jitegemee mfike shuleni pale muone jinsi
serikali yenu inavyowajali wananchi wake kwa kuwasogezea huduma ya elimu kwa
watoto wetu” alisema Massawe.
Pia Shule ya Msingi Ndachi tokea
mwaka 2021 mpaka 2023 imepokea shilingi 125,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa
vyumba vitano vya madarasa ambavyo vimekamilika na vinatumika. “Madawati 50
yametolewa na matundu 12 ya vyoo na chumba kimoja cha ofisi. Shule ya msingi Ndachi
ilikua na changamoto ya vyoo hadi kuna kipindi tulihisi shule inaweza kufungwa
hivyo, napenda kumshukuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma
kufanikisha ujenzi wa matundu 12 ya vyoo kupitia mapato ya ndani” alisema Massawe.
Kwa Shule ya Msingi Mnadani,
alisema kuanzia mwaka 2021-2023 imepokea shilingi 57,000,000 kwa ajili ya
ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ambavyo vimekamilika na vinatumika hivi
sasa. “Kukamilisha darasa moja lililojengwa kwa nguvu ya wananchi, niwapongeze
sana wananchi wa Mtaa wa Mnadani mkiongozwa na Mwenyekiti wenu wa Serikali ya
Mtaa, Ndugu Wawa kwa kujenga darasa moja na sasa serikali imetoa fedha kwa
ajili ya kulikamilisha ujenzi huo, hongerani sana wananchi wa mtaa wa mnadani. Pia,
Madawati 50 ya wanafunzi yalitolewa” aliongeza.
Shule ya Msingi Mbwanga
kuanzia mwaka 2021 hadi sasa fedha zilizotolewa ni shilingi 95,000,000. “Vyumba
sita vya madarasa vimejengwa na vinatumika, matundu 12 ya vyoo yamejengwa na
yanatumika. Mtakumbuka tulikuwa na changamoto ya vyoo, lakini serikali ya mama
Samia Suluhu Hassan imetujengea vyoo vipya na vizuri. Pia tunaishukuru serikali
kwa kutujengea shule mpya shikizi inayojengwa eneo la Matuli kwa kutuletea
shilingi 40,000,000 mapato ya ndani ya halmashauri na jengo hivi sasa lipo
hatua ya upauaji. Shule hii itasaidia sana kwasababu Matuli hakuna shule hivyo,
watoto wanaokaa huko hutembea umbali mrefu kufuata shule ambayo ni Shule ya Msingi
Ndachi, shule hii itawasaidia watoto wanaokaa Matuli kutembea umbali mfupi na
itachochea muamko wa wazazi kupeleka watoto shule” alisema.
Alisema kuwa kata hiyo
inajivunia ongezeko la miundombinu ya Shule ya Sekondari Miyuji kuanzia mwaka
2021 mpaka 2023. Alisema kuwa walipokea shilingi 227,000,000 kwa ajili ya
kujenga vyumba vya madarasa 10, maabara moja ya sayansi, matundu sita ya vyoo
na karo la maji taka. “Serikali inawekeza sana katika sekta ya elimu ikiamini
elimu ni msingi wa maendeleo. Na matarajio yetu mwakani mwezi Januari uandikishaji
wa watoto darasa la awali kuongezeka tunapenda watoto wote wenye umri wa kuanza
shule wawe shuleni kwa sababu shule tunazo za kutosha” alisema Massawe.
Ikumbukwe kuwa Kata ya Mnadani
kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ina jumla ya wakazi 44,311,
kati yao wanawake ni 21,586 na wanaume ni 22,725.
MWISHO
Comments
Post a Comment