Kata ya Mnadani kuwatambua watoto wenye mahitaji maalum

Na. Dennis Gondwe, MNADANI

JAMII imetakiwa kuhakikisha watoto wenye umri wa kuandikishwa shule za msingi wanaandikishwa kwa wakati waweze kupata elimu kwa mujibu wa sheria.

Afisa Elimu Kata ya Mnadani, Robert Tesha akiongea na wananchi


Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Elimu Kata ya Mnadani, Robert Tesha alipokuwa akiongea kwenye mkutano wa hadhara wa wananchi wa Mtaa wa Mnadani katika Kata ya Mnadani jijini Dodoma.

Tesha alisema “zoezi la uandikishaji kwa shule za msingi limeanza tangu mwezi Oktoba mwaka huu. Watoto wanaoandikishwa ni darasa la awali kuanzia miaka minne hadi mitano na darasa la kwanza miaka sita hadi nane na uandikishaji hauna gharama yoyote. Mzazi unapokwenda unatakiwa kwenda na cheti cha mtoto cha kuzaliwa na kama hauna unapitia kwa Afisa Mtendaji wa Mtaa anakuandikia barua na majina kamili ya mwanafunzi kwa sababu majina yanaingizwa kwenye mfumo na hilo jina halitabadilika mpaka chuo kikuu. Niombe sana waleteni watoto tuwaandikishe shule, madarasa yameshajengwa na mama Dkt. Samia Suluhu Hassan sasa hivi tunahitaji watoto tuwaandikishwe na mwisho wa kuandikisha ni tarehe 31 Desemba, 2023 tunapofungua shule tarehe 8 Januari, 2024 ni kusoma tu” alisisitiza Tesha.

Wakati huohuo, alikemea uanzishaji wa shule kiholela katika mitaa ya Kata ya Mnadani. “Niombe huku mtaani katika Kata ya Mnadani kuna vishule vidogo vidogo. Hivyo, haviruhusiwi, lazima uwe na kibali na kusajiliwa, kuna wengine wakiniona wanakimbia, shule za awali kata nzima ya Mnadani zilizosajiliwa ni tano tu, wengine wote hawajasajiliwa. “Naomba tuwaandikishe watoto kwenye shule rasmi. Shule zetu zote za serikali za msingi zina madarasa ya awali, tuwapeleke watoto huko, kwenye shule hizo zenye usajili rasmi, watoto wanapokwenda darasa la kwanza wanajua kusoma na kuandika.” alisema Tesha.

MWISHO

 


Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma