ILEMELA MANISPAA YAVUTIWA UWEKEZAJI MIRADI YA KIMKAKATI DODOMA

Na. Tutindaga Nkwindi, DODOMA

MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela wamevutiwa na uwekezaji na utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kulitaja kuwa ni jiji darasa.


Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Kuruthum Abdallah baada ya kutembelea miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

 

Alisema kuwa wamevutiwa na kiwango cha uwekezaji pamoja na usimamizi madhubuti miradi hiyo na kubainisha kuwa Ilemela inakwenda kutumia uzoefu huo kama darasa. Tunaipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kumiliki na kuendesha miradi mikubwa na yenye tija kama hii. Sisi pia tuna miradi inayofanana na hii. Hivyo, ziara hii imetupa nafasi ya kujifunza mambo mengi ambayo tunaenda kuyafanyia kazi Ilemela ili tuweze kuboresha huduma na kuongeza mapato yetu ya ndani kupitia miradi ya kimkakati alisema Abdallah.

 

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Samson Medda alisema kuwa ushirikiano na kubadilishana uzoefu kati ya halmashauri ni njia muhimu ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kuboresha utendaji wa taasisi za serikali za mitaa. “Tumekuja kujifunza na kuona kwa vitendo namna ambavyo Jiji la Dodoma limefanikiwa kuwekeza katika miradi yenye tija kwa wananchi. Maarifa na uzoefu tulioupata hapa utatusaidia kwenda kuongeza ubunifu, ufanisi na usimamizi bora wa miradi yetu ya maendeleo Ilemela alisema Medda.

 

Nae Diwani wa Viti Maalumu kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Neema Tambi alisema kuwa ziara hiyo iliongeza uelewa mkubwa kuhusu umuhimu wa miradi ya kimkakati katika kukuza uchumi wa halmashauri. Ziara hii imekuwa na manufaa makubwa kwetu kwasababu tumepata ujuzi na uzoefu ambao tutakwenda kuufanyia kazi Ilemela. Tukisimamia vizuri miradi ya kimkakati, tutaimarisha huduma kwa wananchi na kuongeza mapato ya ndani ya halmashauri yetu alisema Tambi.

 

Ziara ya mafunzo ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela katika Jiji la Dodoma ikiangazia miradi ya hoteli, jengo la Kitega Uchumi Mtumba, Bustani ya Mapumziko Chinangali na Soko la wazi la Machinga inajenga taswira chanya ya ushirikiano baina ya mamlaka za serikali za mitaa hapa nchini, huku ikionesha dhamira ya dhati ya viongozi hao katika kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa ufanisi mkubwa ili kuleta maendeleo endelevu.

MWISHO

 

Comments

Popular Posts

Hazina Volleyball yaiduwaza Dodoma Jiji Seti 2-0 Mwenge Super Cup

Dodoma Jiji yaangukia pua dhidi ya Ujenzi Queens Mwenge Super Cup