Miaka minne ya Dkt. Samia, Kizota yanufaika mikopo ya asilimia 10

Na. Coletha Charles, KIZOTA

Wananchi wa Kata ya Kizota, Halmashauri ya Jiji la Dodoma waeleza kunufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa makundi ya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu, ikiwa ni hatua ya kuinua maisha yao kiuchumi na kuimarisha shughuli zao za ujasiriamali.


 

Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Kizota, Theresia Ntui alipokuwa akiongelea mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita.

Alisema kuwa tangu kuanza kwa utolewaji mikopo ya asilimia 10 katika awamu ya sita ya Rais, Dkt. Samia, Kata ya Kizota imenufaika kwa jumla ya shilingi 410,000,000 zilizotolewa kwa vikundi mbalimbali vya kijamii. Alisema kuwa katika fedha hizo, vikundi 28 vya wanawake vilipokea shilingi milioni 192, vikundi 16 vya vijana vilipewa shilingi milioni 164, na vikundi vitano vya watu wenye ulemavu vilipata shilingi milioni 49. “Mikopo hii ni yenye masharti nafuu, haina riba, na inatolewa kwa mtindo wa kikundi. Vikundi hupatiwa muda wa ‘grace period’ inakuwa ni miezi mitatu, ikipita hiyo miezi wanaanza kurejesha mkopo baada ya kutekeleza mradi waliokuwa wanautaka na kikundi kama kikikopa shilingi milioni 10 kitarudisha shilingi milioni 10” alisema Ntui.

Nae, Mwenyekiti wa kikundi cha vijana cha Manyema, Jackson Samwel, alisema kuwa mikopo hiyo imekuwa msaada mkubwa kwa vijana katika kujikwamua kimaisha, na mafanikio ya kikundi chao ni ushahidi tosha kuwa serikali ya awamu ya sita inatekeleza kwa vitendo dhamira yake ya kuwawezesha vijana.

Alisema kuwa mikopo hiyo imewatoa vijana wa kikundi hicho kutoka hali ya utegemezi na kuwa wajasiriamali, ambapo kikundi hicho kina jumla ya wanachama watano ambao wanajihusisha na shughuli za usafirishaji. “Tunatanguliza shukrani zetu za dhati kwa serikali, mbunge wetu na diwani kwa namna walivyotusaidia kupata elimu ya mikopo na hadi kufanikiwa kupata mkopo huu wa shilingi milioni 36. Tumenunua bajaji tatu na pikipiki mbili (bodaboda) na hadi sasa tunamshukuru Mungu tumefanikiwa kuendesha shughuli zetu vizuri na kujitegemea kiuchumi” alishukuru Samwel.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Angel kutoka Mtaa wa Relini, Kata ya Kizota, Edina Mwanjila, alisema kuwa mkopo wa asilimia 10 ni mkopo usio na riba na ambao umekuwa msaada mkubwa katika kuboresha maisha ya wanawake kiuchumi, na kusaidia upatikanaji wa mahitaji ya familia. 

Alisema kuwa kikundi kinajihusisha na shughuli za ushonaji wa nguo (ufundi cherehani) ambapo awali walikuwa na changamoto nyingi za kifedha na vifaa. “Baada ya kupata taarifa kutoka kwa Afisa Maendeleo wa Kata kuhusu mikopo ya asilimia 10, tulielekezwa hatua za kuchukua na tukafuata taratibu, tukaanzisha kikundi, tukasajiliwa rasmi, na hatimaye tukaomba mkopo wa shilingi 3,000,000 kwa wanachama watano. Kupitia mkopo huo, Kikundi cha Angel tumenunua mashine ya kushonea ya ‘overlock’ kwa ajili ya kukamilisha ushonaji wa nguo ‘finishing’, pamoja na vifaa vingine vya ushonaji” alisema Mwanjila.

Ikumbukwe kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan mikopo ya asilimia 10 imeendelea kuwa mkombozi kwa wananchi wa Kata ya Kizota huku wanufaika wakubwa wakiwa ni makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Fursa ya kujikwamua kiuchumi kupitia miradi mbalimbali ya ujasiriamali imekua kichocheo cha maendeleo katika Jiji la Dodoma.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Osterbay Dodoma wajitokeza usafi wa mazingira

Usafi wa Mazingira Kipaumbele Kata ya Chamwino

Wananchi wa Kata ya Mtumba wanufaika na Mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri