Shule ya Sekondari Kikuyu yapongeza ajenda ya Lishe

 Na. Abdul Juma, KIKUYU KASKAZINI

Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za serikali za kuhakikisha chakula na lishe linapatikana katika Shule ya Sekondari Kikuyu na kuwawezesha wanafunzi kusoma wakiwa wameshiba.



Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Shule ya Sekondari Kikuyu, Mwl. Gasper Mmary alipokuwa akiongelea hali ya upatikanaji wa chakula na lishe shuleni hapo yakiwa ni mafanikio ya serikali kwa miaka minne ya serikali.

Alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma imewezesha upatikanaji wa unga zaidi Kilogramu 650 ili kusaidia wanafunzi waliopo shuleni hapo kupata chakula shuleni. “Tunaushukuru mpango huu wa kuboresha chakula na lishe kwa wanafunzi wote wa shule za msingi na sekondari. Katika mpango huu, halmashauri imetusaidia kupata unga zaidi ya Kilogramu 650 ili kuwezesha wanafunzi wote kupata chakula. Suala hili lina mchango mkubwa katika kuwafanya wanafunzi kusoma kwa bidii ili kuweza kupata ufaulu mzuri katika masomo yao” alisema Mwl.  Mmary.

Aidha, Mwalimu wa Taaluma, Mwl. Mwajuma Kidela alipongeza na kuishukuru serikali kwa kuwezesha suala la chakula na lishe kupatikana shuleni hapo kwasababu limekuwa chachu ya wanafunzi kusoma kwa bidii. Alisema kuwa chakula na lishe shuleni hapo imepunguza utoro wa wanafunzi kwa kiwango kikubwa. “Tunaipongeza serikali yetu ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza suala la chakula na lishe shuleni kwasababu jambo hilo katika shule yetu limetuletea manufaa makubwa kwa wanafunzi wetu. Mpango huu umeongeza ufahulu wa hali ya juu ukilinganisha na hapo awali wanafunzi wetu walipokuwa hawapati chakula shuleni” alisema Mwl. Kidela.

Nae mwanafunzi wa Kidato cha Nne, Ratifa Mohamed aliishukuru serikali kwa kuwawezesha kupata chakula na lishe wanapokuwa shuleni kwa lengo la kuongeza ufanisi katika masomo yao hasa yale ya jioni. “Tunaishukuru serikali kwa kutuwezesha kupata chakula na lishe tunapokuwa shuleni. Suala hili linatusaidia sisi wanafunzi kuwa na ufanisi katika masomo yetu ya jioni, tunakuwa na nguvu ya kutosha katika kujisomea. Vilevile, kutoa mchango na ushirikiano katika masuala mbalimbali yanayohusu taaluma, jambo linalosaida kufanya vizuri katika masomo yetu" alishukuru Mohamed.

Chakula na lishe kwa wanafunzi wa shule za sekondari na msingi ni chachu ya ufanisi na ufaulu jambo linaloboresha elimu katika Jiji la Dodoma.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini ni nyenzo ya utendaji kazi serikalini – Dkt. Biteko

JIJI LA DODOMA KUPELEKA MIL 50 ZAHANATI YA KIKUYU

WENZA WA VIONGOZI WASHAURIWA KUANZISHA BUSTANI ZA NYUMBANI