Waziri Mchengerwa atoa Maagizo mahususi kwa Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi
OR. TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais-Tamisemi, Mohamed Mchengerwa amewaelekeza wakuu wa mikoa kuwasimiamia
Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzingatia vipaumbele vya mwaka
2025/26 kikamilifu.
Waziri Mchengerwa alitoa maelekezo
hayo wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara na
taasisi zake kwa mwaka 2025/26.
Alisema kuwa vipaumbele vya
kuzingatia ni kuhakikisha ukusanyaji wa mapato unafikia malengo na kukamilisha
ujenzi wa miundombinu ya afya ya msingi, elimu ya msingi na sekondari kulingana
na mipango iliyowekwa.
Aidha, aliwataka kusimamia
utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidigitali ikiwemo uwekaji na
matumizi ya mifumo na miundombinu ya TEHAMA katika mikoa na mamlaka za serikali
za mitaa ikiwa ni pamoja na vituo vya huduma za afya na elimu.
Vilevile, aliwaagiza kuhakikisha
mapato katika mikoa na mamlaka za serikali za mitaa yanakusanywa kupitia mifumo
ya TEHAMA ya serikali pamoja na kufanya ufuatiliaji wa karibu wa mifumo hiyo
ili kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato.
Alisema kuwa mikoa na mamlaka za
serikali za mitaa zihakikishe zinatekeleza Mikakati ya Uchumi wa Buluu, nishati
safi ya kupikia na mabadiliko ya tabia nchi na utunzaji wa mazingira.
Vilevile, aliagiza mikoa na mamlaka
za serikali za mitaa kuendelea kuimarisha mifumo stahimilivu na endelevu ya
utoaji wa huduma bora za afya, ustawi wa jamii na lishe ili kuboresha huduma
ambayo ni nguzo muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya
kwa wote.
Pia, aliwataka wakuu wa mikoa na
wakurugenzi kuhakikisha watoto walio chini ya miaka mitano wanajiunga kwenye
vituo vya jamii vya kulelea watoto wadogo mchana. “Kila halmashauri itapimwa
utekelezaji wa vipaumbele hivi kwa kuzingatia miradi iliyotengewa bajeti kwa
Mwaka 2025/26” alisisitiza Mchengerwa.
Chanzo: www.tamisemi.go.tz
Comments
Post a Comment