Shilingi Bilioni 7 zatekeleza miradi ya maendeleo Kata ya Miyuji

Na. Coletha Charles, MIYUJI

Diwani wa Kata ya Miyuji, Beatrice Ngerangera, ameipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zaidi ya shilingi bilioni saba kutekeleza miradi ya maendeleo katika kata yake na kusema kuwa miradi hiyo imebadilisha maisha ya wananchi na kuyafanya kuwa bora zaidi.


Kauli hiyo aliitoa alipokuwa akiongea na waandishi wa habari baada ya kutembelea miradi ya maendeleo iliyotekelezwa katika Kata ya Miyuji kwa kipindi cha mwaka 2021-2025 na serikali.

Alisema kuwa serikali imetoa kipaumbele kwa miradi ya Kata ya Miyuji kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi. “Katika kipindi cha miaka minne, kata yetu ya Miyuji imenufaika na miradi yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 7. Hii ni pamoja na ujenzi wa shule ya sekondari yenye miundombinu kamili kuanzia ‘O-Level’ hadi ‘A-Level’, ikiwa na mabweni na nyumba za walimu. Gharama yake ni shilingi 544,000,000 kutoka serikali kuu kupitia SEQUIP” alisema Diwani Ngerangera.

Aidha, alieleza kuwa zaidi ya shilingi milioni 100 zimetumika katika miradi ya ujenzi kupitia fedha za mapato ya ndani za Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Zaidi ya shilingi milioni 400 zilikopeshwa kwa vikundi vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu kama sehemu ya uwezeshaji kiuchumi kupitia mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri.



Kwa upande wake, Mwakilishi wa Wadau wa Maendeleo Mkoa wa Dodoma, Rajabu Juma, alieleza kuwa uwekezaji mkubwa katika elimu umesaidia kupunguza changamoto kama mimba za utotoni ambazo zilikuwa kero kubwa katika kata hiyo. Alisisitiza kuwa maendeleo yanayoonekana ni matokeo ya utekelezaji wa sera za serikali kwa ufanisi.

Miradi iliyotembelewa ni ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Mlimwa ‘C’ na Shule ya Sekondari Miyuji ‘B’, upanuzi wa Zahanati ya Mpamaa, ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita sita inayounganisha Kata ya Miyuji na Ipagala.

Comments

Popular Posts

Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini ni nyenzo ya utendaji kazi serikalini – Dkt. Biteko

JIJI LA DODOMA KUPELEKA MIL 50 ZAHANATI YA KIKUYU

Waziri Mkuu Mgeni Rasmi NBC Dodoma Marathon 2023