SERIKALI YAPONGEZWA KUTOA FEDHA UJENZI WA DODOMA ENGLISH MEDIUM
Na. Dennis Gondwe, IPAGALA
KIONGOZI wa mbio za Mwenge
wa Uhuru mwaka 2023, Abdalla Shaib Kaim ameipongeza serikali ya awamu ya sita ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha za kutekeleza miradi ya
maendeleo ikiwemo elimu nchini.
Pongezi hizo alizitoa
alipoongoza Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 kutembelea, kukagua na kuweka jiwe la
msingi ujenzi wa Shule ya Awali na Msingi ya Dodoma English Medium katika Kata
ya Ipagala jijini Dodoma.
Kaim alisema “niipongeze
serikali ya awamu ya sita kwa kazi kubwa inayofanya ikiwa ni pamoja na kutenga
na kutoa fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maendeleo. Tumejiridhisha na
nyaraka za mradi huu baada ya kuzikagua zipo vizuri sambamba na mradi nikiri
mpaka hatua hii kazi kubwa na nzuri imefanyika. Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka
2023 tumeridhia uwekaji jiwe la msingi” alisema Kaim.
Akisoma
taarifa ya ujenzi wa Shule ya Awali na Msingi ya Dodoma English medium kwa
kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali
na Msingi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prisca Myalla alisema kuwa lengo la
kujenga shule hiyo ni kutoa elimu bora zaidi ambayo itasaidia kupata wataalam
mbalimbali kwa maendeleo ya kiuchumi. “Lengo lingine ni kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, kuongeza
uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la awali na msingi na kuwezesha wananchi wa
kipato cha kati kupata fursa ya kuwapeleka watoto katika shule ya mchepuo wa
kiingereza inayomilikiwa na Serikali” alisema Myalla.
Alisema kuwa
halmashauri ilipokea shilingi 400,000,000 tarehe 20 Aprili, 2023 kutoka
serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa shule ya awali na msingi. Halmashauri ya Jiji
Dodoma imetoa shilingi 58,316,799 kupitia mapato ya ndani kusaidia ujenzi huo. “Ndugu
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023, utekelezaji wa mradi huu ulianza rasmi tarehe 05.05.2023. Tumefanikiwa kujenga Jengo la Utawala, vyumba 11 vya madarasa,
ikiwa madarasa 02 ni kwa ajili ya Elimu ya Awali na madarasa 9 kwa ajili ya
darasa la I hadi la VII. Aidha, yamejengwa matundu 38 ya vyoo, matundu 6 ni kwa
ajili ya wanafunzi wa elimu ya Awali na 32 kwa ajili ya elimu ya msingi. Hadi
sasa mradi upo hatua za umaliziaji. Miti 200 imepandwa kati ya hiyo, Miti 100
ni ya matunda na Miti 100 ni kwa ajili ya kivuli” alisema Myalla.
Akiongelea
gharama za mradi huo, alisema kuwa umetumia shilingi 330,882,100 na unatarajia
kukamilika tarehe 31 Oktoba, 2023.
Kuhusu
mafanikio ya mradi, alisema kuwa utatoa huduma ya elimu ya mchepuo wa
kiingereza na kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule zenye upungufu wa
vyumba vya madarasa. “Mafanikio mengine ni kuleta huduma ya elimu karibu na
jamii, kuongeza ufaulu kwa wanafunzi katika suala zima la kitaaluma kutoka asilimia
89.9 kwa mwaka 2022 na kufikia asilimia 100 na kuhamasisha jamii juu ya
utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti” alisema Myalla.
MWISHO
Comments
Post a Comment