WILAYA YA DODOMA IMEPANDA MITI 4,500,000 KAMPENI YA KIJANISHA DODOMA

Na. Dennis Gondwe, DODOMA

WILAYA Dodoma imefanikiwa kupanda miti 4,500,000 katika kampeni ya Dodoma ya kijani na utekelezaji wa ujumbe wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 unaosisitiza utunzaji wa Mazingira.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 Abdalla Shaib Kaim akipanda mti kwenye mradi wa Maji safi nzuguni


Akisoma risala ya utii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru Wilaya ya Dodoma katika uwanja wa Shule ya Msingi Chamwino, Katibu Tawala Wilaya ya Dodoma, Sakina Mbugi alisema kuwa Wilaya ya Dodoma ipo mstari wa mbele katika kutunza Mazingira. “Katika kutekeleza ujumbe wa Mwenge wa Uhuru wilaya imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika utunzaji wa Mazingira na kuokoa vyanzo vya Maji kwa ustawi wa viumbe hai na uchumi wa Taifa. Katika kipindi cha miaka mitano ya Kampeni ya Dodoma ya Kijani Miti 4,500,000 imepandwa katika maeneo mbalimbali pamoja na chanzo cha Maji Mzakwe. Aidha, wilaya imeweza kusambaza vifaa vya kuhifadhia taka 80 katika barabara na mitaa” alisema Mbugi.

Akiongelea utekelezaji wa agizo la serikali la kupanda miti 1,500,000 alisema asilimia 81 ya miti imepandwa. “Mheshimiwa Rais; Wilaya ya Dodoma katika utekelezaji wa agizo la serikali la kupanda miti 1,500,000 imefanikiwa kupanda miti 1,224,459 sawa na asilimia 81.6 kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji, Mfuko wa Misitu Tanzania, Wadau binafsi na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania” alisema Mbugi.  

Akiongelea uzalishaji taka alisema kuwa Wilaya ya Dodoma inakadiriwa kuzalisha tani 391 za taka ngumu kwa siku. “Kata za nje ya mji huzalisha tani 115 na kata za mjini huzalisha tani 276. Tani 180- 200 zinaondoshwa kwa siku sawa na asilimia 51.2. Wastani wa taka za plastiki tani tano hukusanywa na kurejereshwa kwa siku kupitia vituo vidogo vya ukusanyaji na uchakataji wa taka za plastiki. Wilaya ya Dodoma imeendelea kuhifadhi, kulinda na kuhamasisha matumizi endelevu ya misitu na kufanya doria za mara kwa mara. Elimu juu ya uhifadhi wa misitu na nishati mbadala inatolewa kwa wananchi” alisema Mbugi.

Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 unaongozwa na kaulimbiu isemayo “Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa ustawi wa Viumbe Hai kwa Uchumi wa Taifa”

MWISHO

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma