MWENGE WA UHURU WAZINDUA KITUO CHA AFYA NKUHUNGU- DODOMA
Na. Dennis Gondwe, NKUHUNGU
MWENGE wa Uhuru mwaka 2023 umezindua Kituo cha Afya
Nkuhungu ili kiweze kuwahudumia watanzania baada ya kujiridhisha na ujenzi wa
kituo hicho na nyaraka kufuatia ukaguzi uliofanyika.
Kauli hiyo ilitolewa na Kiongozi wa mbio za Mwenge
wa Uhuru mwaka 2023, Abdalla Shaib Kaim alipoongoza Mwenge wa Uhuru kutembelea
na kukagua ujenzi wa Kituo cha Afya Nkuhungu kilichopo jijini Dodoma.
Kaim alisema kuwa Mwenge wa Uhuru umepita kwenye
Kituo cha Afya Nkuhungu na kusema kuwa ujenzi wake umefanyika vizuri.
“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya pamoja na maelekezo ambayo nimetoa kwa dhati kabisa
na kwa heshima ya Mheshimiwa Rais na wananchi hawa niseme Mwenge wa Uhuru mwaka
huu tumeridhia uzinduzi wa kituo hiki cha afya” alisema Kaim.
Akisoma taarifa ya
ujenzi wa Kituo cha Afya Nkuhungu kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru
kitaifa, Mkuu wa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Dkt. Andrew
Method alisema kuwa halmashauri inatekeleza mradi huo kupitia mapato ya ndani
ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Tamisemi ya kujenga vituo vitatu vya afya
kupitia mapato ya ndani. ”Vituo vingine vinavyojengwa kupitia mapato ya ndani ni Zuzu na
Kizota ambavyo vipo katika hatua ya umaliziaji. Lengo la mradi huu ni kusogeza huduma za
Afya karibu na wananchi wa Kata ya Nkuhungu yenye wakazi 49, 337. Vilevile, kituo
hiki kinahudumia wananchi wa kata za jirani za Kizota yenye wakazi 30,632 na
Mnadani yenye wakazi 44,311 pamoja na kutoa huduma za rufaa kwa Kata za
Chigongwe yenye wakazi 8,933, Nala yenye wakazi 11,715 na Mbalawala yenye
wakazi 11,370” alisema Dkt. Method.
Akiongelea mafanikio ya mradi huu aliyataja kuwa ni kuhudumia
wakazi 49,337 wa Kata ya Nkuhungu. “Vilevile, wakazi 106,961 wa Kata jirani za Kizota, Mnadani,
Chigongwe, Nala na Mbalawala wananufaika na huduma za Afya kupitia kituo hiki.
Wajawazito 5,470 na watoto 20,786 wenye umri chini ya miaka mitano wanatarajiwa
kunufaika na huduma za Afya ya uzazi na mtoto” alisema Dkt. Method.
Kuhusu gharama za mradi, alisema kuwa hadi kukamilika
awamu ya kwanza shilingi 382,996,246 zimetumika zikihusisha ujenzi wa majengo
ya kutolea huduma, kichomea taka na ununuzi wa vifaa. “Ujenzi wa majengo shilingi 322,996,246.00 na
ununuzi wa vifaa na samani shilingi 60,000,000” alisema.
Ikumbukwe kuwa huduma zinazotolewa
baada ya kufunguliwa kwa kituo cha Afya Nkuhungu ni Afya ya uzazi na
mtoto (RCH Clinic) kwa wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano,
huduma za matibabu ya Wagonjwa wa Nje (OPD) na huduma za Maabara.
Mkazi wa Nkuhungu, Mwaimvua Abdallah alisema kuwa
uzinduzi wa kituo hicho cha afya ni ukombozi kwa wanawake waliokuwa
wakilazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma za tiba mjini.
MWISHO
Comments
Post a Comment