WINGI WA WANANCHI NZUGUNI WAMKOSHA MKIMBIZA MWENGE KITAIFA UWEKAJI JIWE LA MSINGI BARABARA YA TARURA
Na. Dennis Gondwe, NZUGUNI
KIONGOZI wa mbio za Mwenge
wa Uhuru mwaka 2023, Abdalla Shaib Kaim amefurahishwa na mamia ya wananchi wa Kata
ya Nzuguni waliojitokeza kwa wingi kuupokea na kuushangilia Mwenge wa Uhuru
ulipofika kuweka jiwe la msingi mradi wa Barabara ya Nzuguni-Mahomanyika.
Kaim alisema “kabla sijatoa
majumuisho ya Mwenge wa Uhuru kukagua barabara hii niwapongeze wananchi wa
Nzuguni kwa namna mlivyojitokeza kwa wingi, haya ni mafuriko makubwa,
shamrashamra na vibe la kutosha kuupokea na kuukimbiza Mwenge wa Uhuru. Hakika
ninyi ni watu wema na wazalendo wakubwa”.
Aidha, alimpongeza Mbunge wa
Jimbo la Dodoma, Anthony Mavunde kwa hamasa yake katika Mwenge wa Uhuru.
“Pongezi kwa Mheshimiwa Mavunde tunakushukuru kwa kazi nzuri pamoja na wingi wa
majukumu uliyonayo lakini umeona umuhimu wa kujumuika nasi. Hongera sana Mungu
akubariki wewe ni mtu bingwa” alisema Kaim.
Akiongelea mradi wa Barabara
ya Nzuguni-Mahomanyika kilometa tano alisema kuwa imejengwa kwa kiwango bora.
“Mbio za Mwenge wa Uhuru tumepokea taarifa ya mradi na Mwenge wa Uhuru umefanya
ukaguzi wa nyaraka mbalimbali na kukagua hatua ya ujenzi wa mradi iliyofikiwa.
Mhe Mkuu wa Wilaya ukaguzi wa kina umefanywa na Mwenge wa Uhuru umejiridhisha
nyaraka zote zipo vizuri, vigezo na ubora umeonekana. Hongera sana Wakala wa
Barabara za Mijini na Vijijini. Mwenge wa Uhuru 2023 umeridhia uwekaji wa jiwe
la msingi mradi huu” alisema Kaim.
Akisoma
taarifa ya ujenzi wa Barabara ya Nzuguni-Mahomanyika Kilometa tano kwa kiongozi
wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2023, Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini
(TARURA) Wilaya ya Dodoma, Mhandisi Emmanuel Mfinanga
alisema kuwa barabara hiyo imejengwa kwa lami ngumu. “Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru
2023; Barabara ya Nzuguni- Mahomanyika ina Kilometa 13 kutoka Nzuguni hadi
kufika Barabara ya Mzunguko wa Nje (Outer Ring road). Kutokana na umuhimu wa
barabara hii, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa mwaka wa fedha
2021/2022 ilitenga fedha shilingi 6,109,748,702 kwa ajili ya ujenzi wa Kilometa
tano za lami ngumu” alisema Mhandisi Mfinanga.
Akiongelea lengo la ujenzi
wa barabara hiyo alisema kuwa utasaidia kupunguza msongamano kwenye barabara
kuu iendayo Morogoro. “Lengo lingine ni kupunguza mafuriko, kuwezesha shughuli za Zimamoto, Mradi
wa Maji Safi kufikika kiurahisi na kupanua mtandao wa barabara kwa kuunganisha
barabara ya Mzunguko wa Nje (Outer ring Road)” alisema Mhandisi Mfinanga.
Alisema kuwa
mradi huo ni wa manufaa kwa wananchi. ”Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa
Uhuru 2023, kukamilika kwa mradi huu kutawezesha shughuli za kijamii kufikika
kirahisi kwasababu barabara hii ni kiungo kikubwa kwenda Mji wa Serikali
(Mtumba), Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, Kituo kikuu cha Mabasi
Dodoma na Soko kuu la Job Ndugai lakini pia wananchi wa Kata ya Nzuguni wapatao 50,454, kufika katika
maeneo yao kirahisi. Pia uwepo wa barabara utawezesha shughuli mbalimbali za
kiuchumi kufanyika na hivyo kukuza uchumi wa jamii na Taifa” alisema.
Gharama za mradi huo ni shilingi 6,109,748,702, na shilingi 5,246,805,322
sawa na asilimia 86 kimelipwa.
MWISHO
Comments
Post a Comment