Baraza la Wafanyakazi Jiji la Dodoma lajadili rasimu ya mapendekezo ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2026/2027
Na. Mwandishi Wetu, DODOMA
Baraza la Wafanyakazi wa
Halmashauri ya Jiji la Dodoma limekutana kujadili taarifa ya utekelezaji wa
shughuli za halmashauri pamoja na rasimu ya mapendekezo ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 ambapo
uongozi huo ulieleza kiasi cha bajeti kinachotarajiwa kutekelezwa katika
kipindi hicho.
Akizungumza katika kikao hicho, Mchumi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Francis Kaunda alisema kuwa halmashauri imekasimia kukusanya shilingi bilioni 166 kutoka vyanzo vyake vya ndani, serikali kuu na wahisani mbalimbali kwaajili ya kutekeleza shughuli za maendeleo, utoaji huduma na kujiendesha.
Kaunda alisema kuwa
kutoka mapato ya ndani kiasi cha shilingi bilioni 73 kinatarajiwa kukusanywa
ambapo kati ya fedha hizo shilingi bilioni 46 ni mapato yasiyolindwa na
shilingi bilioni 27 ni mapato lindwa. Fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi
ya maendeleo na matumizi ya kawaida.
Aliongeza kuwa kati ya
fedha hizo, kiasi cha shilingi bilioni 32 kimepangwa kwa ajili ya miradi ya
maendeleo ikiwemo ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu, afya na
barabara, huku shilingi bilioni 13 zikitengwa kwa matumizi ya kawaida ikiwemo
mishahara ya watumishi na uendeshaji wa ofisi. “Msingi wa bajeti hii ni
kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi na kuhakikisha fedha
zinapelekwa kwenye vipaumbele vinavyogusa maisha ya wananchi moja kwa moja”
Kaunda.
Nae, Katibu wa Baraza la
Wafanyakazi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dennis Gondwe alisema kuwa baraza
linaunga mkono jitihada za uongozi katika kuandaa bajeti inayozingatia
vipaumbele vya maendeleo na maslahi ya watumishi. “Upo umuhimu mkubwa wa
ushirikishwaji wa watumishi katika hatua zote za upangaji na utekelezaji wa
bajeti ili kuongeza uwajibikaji na ufanisi katika kazi. Nawasihi watumishi
kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili
kuhakikisha malengo ya halmashauri yanafikiwa kwa wakati” alisema Gondwe.
Kwa upande wake, Katibu
TALGWU Mkoa wa Dodoma, Audax Stephen aliwataka watumishi kuhakikisha wanafanya
usimamizi madhubuti wa fedha za umma na kuzingatia sheria na kanuni.
Comments
Post a Comment